• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Afueni kwa wakazi Githurai 45 barabara zikiendelea kuboreshwa

Afueni kwa wakazi Githurai 45 barabara zikiendelea kuboreshwa

Na SAMMY WAWERU

KWA muda mrefu miundo misingi kama vile barabara katika mtaa wa Githurai 45 viungani mwa jiji la Nairobi imekuwa kikwazo kutokana na ubovu wake.

Msimu wa mvua hali ya barabara imekuwa mbaya, kiasi cha kutatiza shughuli za usafiri na uchukuzi, hasa kwa wanaotembea.

Mvua inaposhuhudiwa, mitaro ya majitaka imekuwa ikifuja na kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Hata hivyo, wakazi wa mtaa huo na ambao ramani yake inasema upo katika eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu sasa wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia mradi wa uimarishaji wa barabara za mashinani unaoendelea.

Kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja, barabara zimekuwa zikiboreshwa hususan vitongoji vyenye idadi ya juu ya watu.

Mahangaiko ya kutembea kwa wanaoishi katika mazingira ya Shule ya Msingi ya Mwiki, Mt Kenya, Mosque, Chuma Mbili na Reli yametatuliwa kufuatia kuimarishwa kwa barabara.

Maeneo mengine ni pamoja na Mumbi, Progressive, Discovery na Mukinyi PCEA, kati ya mengineyo.

Kwa ushirikiano na Benki Kuu ya Dunia, serikali kuu imekuwa ikikabarati barabara hizo za mashinani.

“Mradi huu unaendelezwa na serikali kuu, kupitia ufadhili wa Benki Kuu ya Dunia,” mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya kipekee.

Mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara akizungumzia wahudumu na wamiliki wa tuktuk Githurai. Uimarishaji wa barabara umewafaa kwa kiasi kikubwa wahudumu hao. Picha/ Sammy Waweru

Aidha, kuna baadhi ya barabara zilizoboreshwa kwa lami na zingine kwa kutumia matofali maalum aina ya Cabros.

Hata ingawa hakueleza kiwango jumla cha fedha kilichotumika kuimarisha barabara zilizolengwa, Bw King’ara alisema kufikia sasa zaidi ya kilomita 7 zimekamilika.

“Zaidi ya kilomita 7 zimewekwa lami na cabros,” akasema mbunge huyo.

Kwa mujibu wa takwimu za ujenzi wa Thika Super Highway, barabara kuu na ya kisasa inayounganisha jiji la Nairobi na mji wa Thika yenye urefu wa kilomita 50, iligharimu kima cha Sh31 bilioni.

Aidha, iliundwa chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu. Ilizinduliwa mwaka wa 2012.

Uimarishaji wa barabara mtaa wa Githurai 45 umesifiwa na wakazi hasa waliowekeza katika sekta ya uchukuzi.

“Barabara zilizokarabatiwa zimesaidia kuboresha huduma za uchukuzi na kufungua mianya ya mapato,” akasema Bw Laban Gitonga, mwenyekiti wa muungano wa wamiliki wa tuktuk na magari madogo aina ya maruti Githurai (GTMA).

Bw Gitonga hata hivyo anaihimiza serikali kuimarisha barabara kuu inayounganisha Githurai na Mwihoko, ambayo hali yake inaendelea kuwa mbovu.

You can share this post!

Safari Rally kuwa na helikopta15, helipadi kuundwa

Chama cha wafanyabiashara wa China nchini Kenya chatoa...