• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Idadi ya vijana kwenye kilimo na ufugaji ni ya chini mno – tafiti za shirika

Idadi ya vijana kwenye kilimo na ufugaji ni ya chini mno – tafiti za shirika

Na SAMMY WAWERU

IDADI ya vijana wanaofanya shughuli za kilimo nchini ni ya chini mno, limesema shirika lisilo la kiserikali (NGO) kutoka Amerika na ambalo huwapiga jeki na kuwahamasisha.

Kwenye ripoti ya utafiti wa hivi karibuni ya Heifer International (HPI) uliojumuisha mataifa 11 barani Afrika, asilimia tisa pekee ya vijana wanafanya ufugaji wa kuku.

Ripoti hiyopia inaeleza kwamba ni asilimia 12 ya idadi ya vijana ndio wanaendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Takwimu hizo zinatia wasiwasi, HPI ikionya endapo hatua mahususi hazitachukuliwa huenda sekta ya kilimo cha ufugaji siku za usoni ikafifia Kenya na Bara la Afrika kwa jumla.

“Hali hiyo ilikuwa bayana katika nchi zote tulizoshirikisha. Mbali na ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa, shughuli zingine za kilimo zilifuata mkondo huo – Idadi ya vijana wanaokiendeleza kuwa ya chini sana. Hili ni jambo linalopaswa kututia wasiwasi, tuungane kuliangazia,” anasema Bw David Ojwang, meneja wa mikakati na programu katika Heifer Kenya.

Huku sekta ya kilimo ikiwa kati ya nguzo kuu za uchumi wa serikali, ikikadiriwa kubuni karibu asilimia 50 ya nguvukazi nchini, Ojwang anasema haja ipo kuwapa vijana motisha kuikumbatia kama njia ya kujiajiri.

“Ninahimiza washikadau katika sekta ya kilimo na sekta zingine husika, tufanye hamasisho la umma na pia kupiga vijana jeki wakumbatie kilimo-ufugaji.

“Tuwasaidie waelewe umri wa kufanya kilimo si wakati wanapostaafu. Tumeona vijana kadha wanaoendeleza kilimo-biashara na ufugaji-biashara baadhi yao wanafanya vyema,” afisa huyo akasema katika kongamalo la HPI, lililoandaliwa jijini Nairobi.

Hafla hiyo na ambayo vyombo vya habari vilitajwa kama asasi husika kusaidia kufanya hamasisho, pia ilitumika kujadili mbinu na mifumo faafu na ya kisasa inayopaswa kukumbatiwa.

Kwa mujibu wa utafiti wa HPI, vijana wengi wanaamini kilimo na ufugaji, kinapaswa kuendeshwa na waliostaafu na waliokula chumvi, wengine wakikumbatia kazi ambazo haziwachoshi kupata hela kama vile uendeshaji bodaboda.

HPI ilitua nchini Kenya 1981, ikilenga kuinua jamii ili kuondoa umaskini na njaa, kupitia kilimo na ufugaji.

Lengo la shirika hilo likiwa kuinua zaidi ya familia 330, 000, sawa na watu 1, 625, 000 moja kwa moja na wanaotegemea waliofaidi, kutoka kwa ufukara kwenye ruwaza yake kufikia 2025, Bw George Odhiambo, mkurugenzi mkuu wa HPI – Kenya, hata hivyo alisema shughuli za kilimo zikikumbatia mifumo ya kuvutia kukiendeleza huenda idadi ya vijana ikaongezeka.

“Licha ya kuwa tunawahimiza waingilie kilimo na ufugaji, tuwape motisha na kuwasaidia kukumbatia mifumo ya teknolojia ya kisasa kupata mazao bora na kuongeza uzalishaji,” Odhiambo akasema, akisisitiza ukosefu wa fedha kama kizingiti kikuu miongoni mwa vijana.

Mkurugenzi Mkuu wa Heifer International (HPI – Kenya) George Odhiambo akihutubu katika kongamano lililoandaliwa jijini Nairobi kujadili mikakati ya namna ambavyo vijana wanaweza kushiriki kikamilifu shughuli za kilimo na ufugaji. Picha/ Sammy Waweru.

Ili kuwashawishi kuhusika kikamilifu kwenye masuala ya kilimo na ufugaji, mwaka huu 2021, shirika la Heifer litaandaa mashindano ambapo wanaolengwa ni vijana kutoka nchi 11 barani Afrika, Kenya ikiwemo.

Droo itakuwa ya makundi manne, jumla ya Sh1.5 milioni pesa taslimu zikiwaniwa na kugawanywa kati ya watakaoshinda.

HPI inalenga kushirikisha vijana wanaoingilia kilimo na ufugaji kwa mara ya kwanza.

You can share this post!

Barcelona wacharaza Eibar na kukamilisha kampeni za La Liga...

JAMVI: Viatu vya urithi wa Uhuru vitatosha Muturi Mlimani?