• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:46 PM
Jombi pabaya kwa kudai mvua ya mafuriko ni adhabu ya Mungu

Jombi pabaya kwa kudai mvua ya mafuriko ni adhabu ya Mungu

CHANGAMWE, MOMBASA

Na JANET KAVUNGA

KALAMENI wa hapa alikemewa vikali na wakazi kwa kudai mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayonyesha ni laana kwa sababu watu wamezama katika dhambi.

Jamaa alikuwa kwenye veranda ya duka ambalo wakazi walikuwa wamejisitiri mvua aliporopokwa na kutaka watu wajilaumu kwa mafuriko ya sasa akisema mvua inayonyesha ni laana kwa kuwa watu wanatenda dhambi kwa wingi.

“Mlitarajia nini isipokuwa laana kama haya mafuriko kwa sababu ya dhambi ambazo watu wanatenda? Na bado huu ni mwanzo tu,” jamaa alisema kabla ya watu kumfokea kwa kufurahia masaibu yao.

“Funga mdomo kama huna la kusema. Wewe ni mmoja wa wanaofurahia watu wakiteseka,” polo mmoja alimweleza jamaa huku wengine wakimshambulia kwa maneno ndipo akalazimika kunyamaza.

***

Demu aalika wanaommezea mate kujitetea

BANANA, KIAMBU

Na TOBBIE WEKESA

KIDOSHO wa hapa alizua gumzo kali kwa kuwaalika wachumba wake wote nyumbani kwao wajitetee mbele ya wazazi wake.

Inadaiwa kidosho alichukua hatua hiyo ya kipekee ili kuwapa makalameni nafasi ya kujitetea na kujinadi mbele ya wazazi wake.

Kulingana na mdokezi, kidosho aliamua kufanya hivyo kama njia moja ya kuepuka mzozo miongoni mwa makalameni wakimpigania.

“Nina uhakika hamjuani. Nyinyi nyote mnataka kunioa. Wazazi wangu ndio hawa. Kila mmoja wenu ajitetee,” kidosho aliwaeleza.

Penyenye zinasema makalameni walionekana kuchanganyikiwa. Kila mmoja asijue aanzie wapi.

“Atakayewashawishi wazazi wangu bila shaka nitakuwa wake. Sitaki mwanamume mwenye mzaha katika ndoa,” kidosho alieleza kisha makalameni wakaondoka akabaki mmoja.

***

Polo na mkewe wasutwa kwa kugawana watoto ili kila mmoja awajibike

NDANAI, SOTIK

NA NICHOLAS CHERUIYOT

JOMBI na mkewe eneo hili walisutwa vikali na jamaa zao kwa kugawana watoto ili kila mmoja apambane kushughulikia walio upande wake.

Penyenye zinaarifu kwamba wawili hao walikuwa wakitofautiana kila mara, kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kukosa kushiriki ipasavyo kushughulikia mahitaji ya familia.

“Juzi, mtu na mkewe waliamua kugawana watoto wao watano. Watoto weusi tititi waliachiwa baba na mama akakubali kuwajibikia wengine vilivyo,” mdaku akaeleza.

Jamaa wa familia walipojua, waliingilia kati na kuwaambia kuwa uamuzi wao ni hatari na kuwataka kushirikiana pamoja kutimizia watoto mahitaji yao.

  • Tags

You can share this post!

Maisha ya wanaume yanaendelea kuwa mafupi tangu mlipuko wa...

Uchumi uko sawa mpuuzeni Raila, Ruto aambia Wakenya

T L