• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Krismasi: Alivyorambwa kwenye baa akijigamba mbele ya mahasla ana pesa

Krismasi: Alivyorambwa kwenye baa akijigamba mbele ya mahasla ana pesa

NA MWANGI MUIRURI

KALAMENI aliyejigamba alivyo na pesa mbele ya kundi la mashabiki wa pombe kwenye baa Mjini Makutano, Embu huku akijinunulia vileo kwa wingi, alionyeshwa cha mtema kuni walipomgeuka, wakamvamia na kumpora.

Duru zinaarifu, wakati wa maadhimisho ya Krismasi 2023 jamaa alitua kwenye baa na katikati ya mahasla ambao hawakuwa na chochote akaagiza vikombe vikubwavikubwa vya pombe aina Black Keg.

Polo aliyeingia katika baa moja ya mjini Makutano Kaunti ya Embu siku ya Krisimasi na akaanza kujinunulia vikombe kubwakubwa vya kileo huku mahasla wakiwa wamemzingira bila form yoyote alikiona cha mtema kuni walipomvamia na kumpora.

“Nitilie Keg kikombe kikubwa,” jombi aliagiza, huku akitoa noti ya Sh200.

Kiwango hicho cha pombe kinauzwa Sh70 kwa mujibu wa bei ya baa hiyo, na polo aliambia weita ambaye ni kipusa aweke chenji.

Kilichoghadhabisha mahasla ni alivyozungumza kwa maringo na madaha, akijigamba kwamba ana hela kama njugu.

“Aliingia mfukoni akatoa buda la noti…Akatangaza kuwa alikuwa na Sh12, 000 ambazo alikuwa ameuza mahindi mabichi na alikuwa mtaani kujituliza uchovu wa kulima,” akasema mdokezi wetu.

Licha ya mahasla hao ambao walikuwa wanane kumsihi awanunulie angalau kila mtu kikombe kidogo cha mvinyo, alikataa na kuwashauri waende shambani wamwage jasho kama alivyofanya ili wapate hela za kutesa mtaani.

“Baada ya kusema hivyo kwa maringo makuu, aliagiza vikombe 10 vijazwe na aletewe huku hata akitumana atafutiwe mrembo wa mtaani aponde raha akisema kwamba msimu wa sherehe ulikuwa umefika,” akasema mdokezi wetu.

Polo anasemwa kwamba jinsi ulevi ulivyokuwa unamshika, ndivyo alikuwa akizidisha majivuno na hotuba za kudunisha mahasla hao ambao nao mate yalikuwa tu yakiwatiririka kwa tamaa ya pombe.

“Ndipo mmoja wa mahasla hao alisimama wima akiteta sana kwamba licha ya kuwa maskini, alifaa kupewa heshima na polo huyo pasipo kuzomewa akiitwa mzembe.

Alimshika mashati, wengine wakimrukia na wakamnyanyua juujuu, baadhi yao wakinywa pombe iliyokuwa mezani. Kurejeshwa chini, hakuwa na chochote mfukoni,” mdaku wetu akaarifu.

Mahasla hao walianza kumnunulia pombe kwa hela zake, wasijue chuma chao ki motoni.

“Lakini kumbe mwenye baa alikuwa ameita polisi na kuwaambia kulikuwa na ukora ndani ya biashara yake! Muda si muda polisi walifika na kuwatia mbaroni mahasla hao wote ambao walikubali haraka kurejesha pesa walizokuwa wamesalia nazo,” Meza ya Dondoo Dijitali ikadokezewa.

Isitoshe, walipigia jamaa zao simu wawatumie hela zingine ili polo arejeshewe pesa zake zote.

Polisi nao, walimgeukia wakimpa msomo – Kumshauri siku nyingine asitue kwenye baa na hela mfukoni na kuringia watu walio na kiu cha pombe, hasa ikiwa hawana pesa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Jinsi vijana wanne walivyouawa Buruburu kwa kumiminiwa...

Ujenzi wa daraja la kidijitali kupima uzani wa magari

T L