• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Shakira, aliyeachwa na Pique, atemana na nguli wa magari Lewis Hamilton

Shakira, aliyeachwa na Pique, atemana na nguli wa magari Lewis Hamilton

Na CHRIS ADUNGO

MWANAMUZIKI Shakira Isabel, 46, aliyekuwa mchumba wa mwanasoka mstaafu Gerard Pique, ametemana sasa na dereva maarufu wa magari ya Langalanga, Lewis Hamilton, 38.

Mnamo Julai, Shakira aliungama kuwa “anakaribia kupata hifadhi mpya ya penzi lake kwa Hamilton” baada ya kuanza kuonekana mara kwa mara na dereva huyo wakiponda raha na kuhudhuria mashindano na hafla nyingi pamoja.

Ingawa awali walikuwa wamejaribu kuzima uvumi kwamba wanachumbiana, penzi kati ya Shakira na Hamilton lilianza kujidhihirisha wazi baada ya kukamilika kwa mashindano ya British Grand Prix yapata mwezi mmoja uliopita.

Mrembo huyo alisafiri kwa ndege kutoka Amerika hadi Uingereza kwa lengo la kutazama Hamilton aliyeambulia nafasi ya tatu kwenye kivumbi hicho cha Formula One.

“Mapenzi yana ajabu yake. Hisia zipo na nimeanza kuvutiwa tena na mambo ambayo Pique alifanya niyachukie. Nakaribia kupata mchumba mpya na mtamjua,” akasema Shakira wakati huo.

Hata hivyo, mwanamuziki huyo raia wa Colombia amebwagana sasa na Hamilton baada ya kutofuatiana kuhusu mpango wa kuanza familia na hatimaye kupata watoto pamoja.

“Kubwa zaidi katika mpango wa Hamilton kwa sasa ni kutulia katika ndoa na kupata watoto na mrembo huyo ambaye atakubali kufunga naye pingu za maisha,” akatanguliza mnajimu raia wa Jamhuri ya Domican, Nino Prodigio, ambaye ni rafiki na msiri wa Hamilton.

“Hata hivyo, yaonekana Shakira amekataa kwa kuwa hana mpango wa kupata mtoto tena. Hofu ni iwapo watatengana kabisa au watasalia marafiki na kufikiria kuwa washirika wa pamoja kibiashara,” akaongezea Prodigio kwa kukiri Hamilton aliwahi pia kutoka kimapenzi na warembo Nicole Scherzinger, Rihanna, Rita Ora na Kendall Jenner.

Shakira alitemana na beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Pique, mnamo Juni mwaka jana baada ya kuwa pamoja katika ndoa kwa miaka 12 na kujaaliwa watoto wawili wa kiume – Milan na Sasha.

Mara ya mwisho kwa Shakira kuonekana peupe na Hamilton ni mwanzoni mwa mwezi jana wakishiriki chakula cha jioni katika mkahawa mmoja jijini Barcelona.

Alipakia kwenye Instagram baadhi ya picha walizopigwa na Hamilton akaandika chini ya mojawapo: “Huyo ni kipusa ambaye nitakuwa nikimvisha pete ya ndoa wakati wowote kuanzia sasa.”

  • Tags

You can share this post!

Ruto kurejea tena kunyonga ‘payslips’ za Wakenya

Tanzania yatesa soko la kitunguu kwa ‘kususia’...

T L