• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Tanzania yatesa soko la kitunguu kwa ‘kususia’ kilimo

Tanzania yatesa soko la kitunguu kwa ‘kususia’ kilimo

NA MWANGI MUIRURI

WAKULIMA, madalali na wachuuzi wa kitunguu nchini wanaendelea kuvuna pato la juu lililoongezeka hadi kwa asilimia 875 tangu Februari.

Kilo moja ya aina ya kitunguu chekundu ilikuwa ikinunuliwa kwa Sh20 mwezi wa Februari lakini kwa sasa ni Sh195 katika maeneo mengi ya nchi.

Wanapovuna vinono, ni kilio kwa watumizi bidhaa hiyo katika mapishi, wakiweno wawekezaji wa biashara ya hoteli ambao wamepunguza kitunguu katika chakula hivyo basi kudhoofisha ladha.

Katika soko la Parklands ambalo ni maarufu kwa wateja wa Kihindi, hali si hali wachuuzi wakiteteswa na wateja hao kwa kutomakinikia wingi wa bidhaa hiyo sokoni.

Bw Mbatia Njanjo ambaye ni mchuuzi alilalamika kwamba wanaowaletea bidhaa hiyo sokoni kwa sasa hawatimizi mahitaji ya wateja “hasa hawa wa Kihindi ambao wanapenda kitunguu kama uhai”.

Bw Njanjo alisema kwamba Wahindi hupenda kitunguu na kwa sasa hali halisi ilivyo sokoni, inaonekana kama njama ya kuwalazimisha kutalikiana na ladha wanayoienzi ajabu.

“Bei hiyo imekuwa ikipanda ghafla hapa nchini kutokana na uhaba mkubwa uliosababishwa na ukame na pia kujikokota kwa uagizaji kutoka nchi jirani ya Tanzania,” akasema Bw James Kimani ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kiawara, Kaunti ya Nyeri.

Mji wa Kiawara Kaunti ya Nyeri ndio ngome ya kitunguu na kwa sasa kile chekundu ni adimu. Hapa wateja wanaonekana wakipiga msasa kile cheupe ambacho bei yake kwa sasa ni sawa na ya dhahabu. PICHA | MWANGI MUIRURI

Soko la Kiawara ndilo ngome kuu ya biashara ya kitunguu ambapo mataifa jirani hukongamana huku madalali wakidhibiti bei kulingana na hali ya mavuno.

“Kuna ama kitunguu cha rangi nyekundu au kitunguu cha rangi nyeupe… Acha tuzingatie cha rangi nyekundu kwa kuwa ndicho hupendwa zaidi na ambacho bei yake imekuwa ikiruka juu kwa njia inayoweza ikatajwa kuwa ya kiholela,” Bw Kimani asema.

Aliibua madai kwamba taifa la Tanzania ndilo hupea masoko kitunguu cha ubora wa hali ya juu lakini wakulima wengi wa taifa hilo ni kama wamesusia kilimo hicho hivyo basi kusababisha mfumko wa bei ya kitunguu sokoni.

Kitunguu kinachokuzwa nchini Kenya husemwa kuwa na maji mengi hivyo basi kuoza haraka katika soko.

Lakini hicho chenye maji mengi hurejelewa kama bora zaidi katika utengenezaji wa kachumbari kwa kuwa unyevu huo huja na wingi wa makali katika ladha.

Bw Kimani alisema kwamba bei iliyoko kwa sasa ndiyo ya juu zaidi “kuwahi kututembelea na ijapo sio maombi mazuri kwa wengi, afadhali ukame ambao umedumu nchini kwa zaidi ya miaka miwili uendelee na pia uagizaji hafifu kutoka kwa wakulima wa Tanzania udumu ndio wale wanawekeza mtaji kwa kilimo cha kitunguu waendelee kufurahia pato sokoni”.

Baada ya ukame kukumba maeneo mengi ya nchi, wakulima wengi wa kitunguu waliokuwa wamepata hasara kubwa katika msimu wa Oktoba hadi Desemba waliogopa kupanda mmea huo wa mazao.

“Lakini wale wachache waliothubutu kupanda katika msimu wa mvua ya Aprili hadi Juni ndio hawa sasa ambao pato limewashtua kwa utamu na wingi,” akasema.

Kwa sasa, madalali wamefurika kwenye mji wa Kiawara wakitegea kila aina ya kitunguu watakachopata.

Baadhi ya wateja wametoka katika mataifa kama Burundi na Ethiopia.

“Huku kumejaa madalali wa kutoka nchini Uganda, Rwanda na Sudan Kusini. Wamekuja kununua vitunguu ili wakauze kwa faida. Kwa mkulima, bei ni Sh195 na hata hatuamini kwamba ni sisi tunahesabiwa pesa kiasi hicho,” akasema Bi Faith Mugure, mkulima.

Malori yaliyo na usajili wa mataifa jirani yanaonekana mara kwa mara katika barabara za Kiawara yakisaka vitunguu huku wakulima walio na ufahamu wa kukwamilia mavuno yao wakisababisha uhaba wa muda na kusukuma bei juu.

“Ninyi ambao hamjui kuingia shambani kujichafua sasa fungueni mikoba yenu mtupe fidia ya kuwalimia. Ni wakati wetu sasa na hii bei naona ikitinga Sh250 kwa kilo katika wiki chache zijazo,” akasema Bw Kiago Njiraini.

Hata hivyo, wakulima wengi walitoa malalamiko kuhusu gharama kubwa ya uzalishaji huku kwa mfano, kilo moja ya mbegu kwa sasa ikitinga Sh70,000.

Ekari moja ya mimea ya kitunguu chekundu iko na uwezo wa kutoa kilo 16,000 za mavuno, kwa sasa hili likiwa ni pato la Sh2.4 milioni ikilinganishwa na Sh320,000 ambazo mkulima angepata Februari.

  • Tags

You can share this post!

Shakira, aliyeachwa na Pique, atemana na nguli wa magari...

Sababu ya Sakaja kukataa kuendesha baiskeli na Mama wa Taifa

T L