• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Ababu ashambuliwa na wenzake UDA kwa “kutelekeza wanariadha” 

Ababu ashambuliwa na wenzake UDA kwa “kutelekeza wanariadha” 

Na WANGU KANURI

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba ameshutumiwa vikali na viongozi katika chama cha United Democratic Alliance, kwa kile wanachosema ni kutelekeza wanariadha nchini.

Viongozi hao wamemnyooshea kidole cha lawama Bw Namwamba kwa “kuruhusu maafisa wa Wizara ya Michezo kusafiri katika starehe na wasichana” badala ya wanariadha katika safari kuelekea jijini Budapest, Hungary kwa mashindano ya Riadha za Dunia yalioanza Agosti 19 yakitarajiwa kukamilika Agosti 27, 2023.

Wa hivi punde zaidi kumkashifu Waziri Namwamba ni Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Gladys Boss Shollei aliyemtaka aelezee kwa nini mradi wa Talanta Hela bado haujaanza kufanya kazi licha ya kudai kwamba upo tayari.

“Niliangalia jana (Agosti 21, 2013) hiyo Talanta Hela App wala haipo. Na walikuwa wametuambia washaizindua tayari,” akasema Bi Shollei.

“Siku ile nyingine wakati kikosi cha Kenya kilienda Tunisia kwa michezo ya ufukweni, kilikuwa kimevalia sare feki labda hata zilinunuliwa River Road. Kufikia wakati wanariadha wanaowakilisha taifa wanavalishwa jezi feki inamaanisha kuna kasoro,” akaendelea kushambulia.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah kwenye matamshi yake bungeni, alimlaumu Bw Namwamba kwa kutoshughulika na wanariadha licha ya juhudi zao za kushinda medali mbalimbali.

“Haukuteuliwa waziri ili uzunguke na bendera ya Kenya garini mwako huku ukinyanyasa wananchi kwenye trafiki ukiwa umeandamwa na magari nyuma yako. La! Uliteuliwa kuwahudumia watu walio kwenye wizara yako,” akasema.

Akielezea kusikitishwa na tabia za Bw Namwamba, Bw Ichung’wah, alisema kuwa cha kushangaza sana ni kuwa wanariadha hao hushindia nchi medali lakini hakuna msimamizi yeyote kwenye Wizara ya Michezo au hata waziri mwenyewe atawalaki wanapofika kwenye uwanja wa ndege.

“Hata kuwashukuru kwa kazi nzuri wanayofanya. Iwapo wewe ni waziri wa michezo, kazi yako ni kuwasaidia wanamichezo hata wale walio na ulemavu.”

Akiongezea, Bw Ichung’wah alisema kuwa Waziri Namwamba ataitwa bungeni ili kueleza ni kwa nini hana muda wa kuwashughulikia wanamichezo ilhali ni jukumu lake.

“Kazi yake si kuwapeleka watu wanaosafiri bure nchi za nje bila majukumu yoyote huku wanariadha wakiachwa,” akasema.

Akiafikiana na Bw Ichung’wah, Seneta wa Nandi Samson Cherargei pia alimshutumu Waziri Namwamba akisema kuwa anaendelea kufuja pesa za wizara hiyo kwa starehe.

Akiandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), Cherargei, ambaye pia ni mwanasiasa wa UDA, alisema, “Kivipi wakuu katika wizara hiyo watasafiri kwa starehe na wapenzi wao mpaka Riadha za Dunia nchini Hungary badala ya wanariadha wetu?”

Kisha akaongezea, “Wanariadha wetu wa kike wananyanyaswa kimapenzi na kifedha. Bunge sharti imwite Waziri wa Michezo ili tuepuke usimamizi mbaya wa michezo yetu.”

Hata hivyo, Taifa Dijitali imebaini kwamba Waziri Namwamba hakusafiri kuelekea Budapest, Hangary kama alivyodai Seneta Cherargei na badala yake katika tarehe inayodaiwa alifanya hivyo, alikuwa nchini kwa michezo ya CASA mjini Nakuru.

  • Tags

You can share this post!

Waliowekeza karibu na kwa Pasta Ezekiel wakadiria hasara

DONDOO: Mke amchemkia mumewe kwa ‘kumla’ kisura...

T L