• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 2:31 PM
Aililia mahakama asukumwe jela ili apate mlo wa bure

Aililia mahakama asukumwe jela ili apate mlo wa bure

NA BRIAN OCHARO

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 32 ameiomba Mahakama ya Mombasa kumsukuma gerezani mara moja ili aweze kupata chakula cha bure katika kisa ambacho kimeweka wazi hali mbaya ambayo Wakenya wengi wanakumbana nayo kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Bw Hamisi Munyoki, ambaye alifikishwa mbele ya mahakama hiyo kwa shtaka la kuharibu mali, alikiri shtaka hilo na kuiomba mahakama imfunge ili apate chakula cha bure.

Munyoki alishtakiwa kwa kuvunja mlango wa kioo wa thamani ya Sh170, 000 ambayo ni mali ya Ali Shali Ali.

Alidai kufanya kosa hilo katika kampuni ya Lotas Automotive Kenya Ltd mnamo Agosti 30, 2023.

Mahakama ilielezwa kwamba Munyoki ambaye alionekana kuchanganyikiwa aliokota mawe na kuvunja mlango huo wa kioo, na kusababisha uharibifu mkubwa.

Akielezea kukata tamaa kwake, Munyoki alisema kuwa alichoka kujaribu kujiua baada ya jaribio la kwanza kufeli, ambapo aliruka ndani ya Bahari ya Hindi kufa.

“Kusema ukweli naomba unisaidie kwa kunipeleka gerezani ili nipate chakula cha bure ili niendelee kuishi, mawazo haya ya kujiua si mazuri, awali nilijitupa baharini lakini sikufa, niliokolewa na kukamatwa,” alisema.

Munyoki, ambaye alisema alizaliwa Mombasa lakini kwa sasa anaishi Utawala Mavoko, Kaunti ya Machakos, alisisitiza kuwa yuko tayari kufanya kazi akiwa gerezani na kuiomba mahakama kumpatia chakula kingi.

“Ninaishi peke yangu, sina wanafamilia wowote pamoja nami. Sina mke. Nilikuwa na mke kwa jina Elizabeth Gitau, lakini tulitengana, na sasa ameolewa. Ninahitaji chakula tu, Nitashirikiana vyema na askari wa gereza,” alisema.

Munyoki alikiri kwamba alisafiri hadi Mombasa kwa ajili ya kujitoa uhai kwa kujirusha katika Bahari Hindi.

“Unaweza kuona mtu anahangaika katika dunia hii, lakini si kwa kupenda kwake. United Democratic Alliance (UDA) ilitakiwa kunipa pesa, lakini haikufanya hivyo,” alisema.

Munyoki aliihakikishia mahakama kuwa yuko sawa kiakili na kuwa ataonyesha tabia nzuri wakati akitumikia kifungo chake na kufurahia milo ya bure.

Hata hivyo, Hakimu Mkuu Mkazi Rita Orora hakushawishika kuwa Munyoki alikuwa na akili timamu na akaahirisha kutoa hukumu hadi mahakama ihakikishe hali yake ya kiakili.

“Mshukiwa atafanyiwa tathmini ya kiakili kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yake,” alisema hakimu huyo.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 11.

 

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Chali akikuvunja moyo mteme mara moja, la...

Harusi yetu tuliita watu 50 pekee, si uchoyo, ni vile...

T L