• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 8:50 AM
PENZI LA KIJANJA: Chali akikuvunja moyo mteme mara moja, la sivyo utajuta!

PENZI LA KIJANJA: Chali akikuvunja moyo mteme mara moja, la sivyo utajuta!

NA BENSON MATHEKA

VIDOSHO, komeni kukwamilia machali wanaowavunja moyo na kuwatesa kwa tabia zao chwara.

Kwa nini ujisononeshe sababu ya kudekeza dume eti atabadilika jinsi unavyodhani?

Kukwamilia naye ni kujitumbukiza katika mateso na kujifunga mnyororo wa utumwa utaishi kubeba zigo la tabia zake.

Ingawa baadhi ya wanaume wanaweza kusamehewa kwa makosa wanayofanyia wapenzi wao, ni vigumu kubadilisha dume lililokomaa.

Jinasue kutoka kwa mwanamume kama huyo asivuruge maisha yako na kukunyima furaha.

“Muache na ufunge huo mlango milele kwa kutupa ufunguo katika bahari ya sahau. Usiruhusu mwanamume abomoe heshima yako,” ashauri mwanasaikolojia Betty Wangai.

Wangai anashikilia kwamba mwanamume anayedhalilisha mwanadada kamwe hatakoma tabia hiyo, kumkwamilia ni tikiti ya kukutamausha.

“ Iwapo mwanamume anakufokea na kukugombeza, ukimvumilia ataendelea kufanya vivyo hivyo. Ikiwa mwanamume hakuthamini, hatajifunza jinsi ya kukutunza kama kito hata ukiishi maisha yako yote ukimnyenyekea,” asema Wangai.

Wanaume wanafaa kufanya wapenzi wao wahisi wanathaminiwa katika uhusiano kwa kuwapa fursa ya kuchangia maoni na kufanya maamuzi ya nyote wawili. Iwapo mwanamume hafanyi hivyo, basi hatoshi mboga.

“Hii ni kwa sababu kuna vitu ambavyo haviwezi kufunzwa mtu maishani,” asema na kuhimiza wanaume wajitume kujifunza jinsi ya kutunza, kuthamini na kudekeza wapenzi wao.

“Uadilifu, huruma, upendo, uaminifu, kujitolea, kujinyima, nidhamu ya kifedha na maadili mengine yote ambayo humfanya mwanamume kuwa mtu wa heshima; hayana darasa la kufundishwa, mtu anajifunza tangu utotoni,” anaeleza Wangai.

Itakuwa kujiumiza iwapo utampa mwanamume nafasi ya pili kila akipungukiwa na mambo kama ya kimsingi.

Ukigundua chali hajali maadili haya na mengine muhimu kwako, fanya hima toroka na urudi soko.
Ukifunga ndoa na mtu kama huyo utakuwa umejisulubisha na daima maisha yako yatajaa masononeko.

“Nahimiza vipusa hivi, iwapo kuna mtu anayehitaji nafasi ya pili ni wewe. Sio ibilisi la dume unalosubiri libadilike kuwa malaika, utasubiri hadi kaburini,” anaonya Ruth Odili, mtaalamu wa masuala ya mahusiano ya kimapenzi.

“Ikiwa unafikiri utaweza kubadilisha mwanamume mliyekutana akiwa na umri wa miaka 30, unajidanganya. Huyo sio samaki umkunje angali mbichi, katika umri huo wa utu uzima tayari ameshachagua anavyotaka kuwa maisha yake. Wala hakuna unachoweza kufanya abadilike,” Odili anasisitiza.

Naye Wangai anahitimisha kwa kuhimiza vipusa wawe jasiri wa kujinasua kutoka wanaume wa aina hiyo na “kumtakia kila heri demu atakayejipata na chali wa sampuli hiyo”.

  • Tags

You can share this post!

Wazee Mlima Kenya wataka waruhusiwe kutembea na visu,...

Aililia mahakama asukumwe jela ili apate mlo wa bure

T L