• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:47 AM
Aliyekuwa afisa wa NMS asimulia machungu ya maisha

Aliyekuwa afisa wa NMS asimulia machungu ya maisha

NA WINNIE ONYANDO

AFISA wa zamani wa lililokuwa Shirika la Kusimamia Jiji la Nairobi (NMS) sasa anakabiliwa na hali ngumu ya maisha huku akisubiri serikali ya gavana Johnson Sakaja kutimiza ahadi iliyotoa baada ya uchaguzi.

Maisha ya Samuel Mbugua, 25, yanazidi kuwa mabaya huku akikabiliana na matatizo ya kifedha akisubiri malimbikizo ya malipo yake ya miezi saba aliyofaa kupokea kutoka kwa serikali ya kaunti.

Mbugua ni miongoni mwa maafisa 700 ambao walihudumu chini ya NMS.

Akizungumza na Taifa Leo, Mbugua alifichua matatizo anayopitia.

“Naishi Gachie Delta. Kodi yangu ya nyumba ni Sh7,000 kwa mwezi. Hata hivyo, landledi alinifungia nje mimi na familia (kwa sababu ananidai Sh49,000) na tukalazimika kulala kwenye kituo cha petroli kilichokuwa karibu.” Mbugua aliambia Taifa Leo.

Mbugua alifichua anafaa kulipwa Sh171,460.

Licha ya changamoto zilizomkabili tangu mkataba wake kusitishwa ghafla, Mbugua bado yuko imara huku akiwa na matumaini kuwa watalipwa mishahara yao.

“Naomba serikali itulipe. Kwa sasa maisha yamekuwa magumu zaidi,” akaongeza Mbugua.

Hata hivyo, Wabuyabo Flavian Alex, Mwenyekiti wa Maafisa wa NMS, amekuwa mwanga wa matumaini kwa maafisa hao ambao kwa sasa wanashindwa kujikimu.

“Nimejaribu leo asubuhi kuingilia kati suala hilo na hatimaye mmiliki wa nyumba alikubali kumpa muda wa wiki mbili. Tunahisi kwamba serikali ya gavana Sakaja imetutelekeza,” akasema Bw Wabuyabo.

“Hatujalipwa mshahara wa miezi saba baada ya mkataba wetu kusitishwa kinyume cha sheria.”

Mapema mwaka huu 2023, gavana Sakaja aliagiza wafanyikazi wa zamani wa NMS ambao mkataba wao uliisha kuripoti City Hall, na kutuma upya maombi ya kazi.

NMS ilianza kufanya kazi kufuatia makubaliano ya kisiasa kati ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo shughuli kadhaa za kaunti zilichukuliwa saini na serikali ya kitaifa.

Kwa hivyo, rais huyo wa zamani alimteua Jenerali Mohammed Badi kama mkuu wa NMS, kundi la maafisa wanaotoa huduma kwa Serikali ya Kaunti.

Muda wa uongozi wa Badi uliisha kwa kuchaguliwa kwa Johnson Sakaja mnamo Agosti 2023, lakini hatima ya wafanyikazi wa NMS bado haijulikani.

  • Tags

You can share this post!

Man-City wapewa mswaki katika makundi ya UEFA

El Nino huenda isigonge Nyeri sana, mtaalamu afichua

T L