• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
El Nino huenda isigonge Nyeri sana, mtaalamu afichua

El Nino huenda isigonge Nyeri sana, mtaalamu afichua

WINNIE ONYANDO Na SAMUEL MAINA

MKURUGENZI wa Idara ya Hali ya Hewa katika Kaunti ya Nyeri, John Muiruri, amesema huenda El Nino ikakosa kugonga sana kaunti hiyo.

Mtaalamu huyo alisema kuwa atatoa ripoti kamili wiki ijayo kuhusu mafuriko na maporomoko ya ardhi yanayotarajiwa katika eneo hilo.

“Utabiri wa hali ya hewa wa kitaifa ulitolewa Jumatano na baada ya hapo, tukaanza mchakato wa kutabiri hali itakavyokuwa katika kila kaunti. Hata hivyo, itabidi tusubiri hadi wiki ijayo ili nitoe ripoti kamili,” akasema Bw Muiruri.

Mapema mwezi huu, Bw Muiruri alidokeza uwezekano wa Nyeri kukumbwa na mvua nyingi kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, alisema Idara itatoa ripoti ya kina kuhusu mvua za Oktoba-Novemba-Desemba mara watakapokamilisha uchunguzi wao.

“Bado hatujapokea utabiri wa Oktoba -Novemba -Desemba na bado tunafuatilia hali kwa sababu tunaona dalili za kuwa na El Nino. Kwa hivyo kwa sasa, siwezi kusema tutapokea mvua kiasi gani,” akaongeza mtaalamu huyo.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi mnamo Agosti 30, 2023, Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa David Gikungu alisema mvua kubwa inatarajiwa kunyesha katika eneo la Ziwa Victoria, kaunti za Kisii, Elgeyo Marakwet, Bungoma, Trans Nzoia, Pokot Magharibi, Vihiga, Laikipia, Nakuru na Narok.

El Nino hutokea wakati ambapo maji kwenye bara ya Pasifiki Pwani mwa taifa la Peru, huchemka, huzua joto na kubadilisha hali ya hewa katika nchi mbalimbali ulimwenguni. Hali hii ndiyo husababisha mvua kubwa ukanda wa Afrika Mashariki hasa kuanzia Oktoba-Novemba na Desemba.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa afisa wa NMS asimulia machungu ya maisha

Ogina Koko alenga kuwa Rais akiahidi kuondoa Januari kwenye...

T L