• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
CECIL ODONGO: Teuzi za Rais Ruto za Makatibu wa Wizara hazikuzingatia usawa wa kimaeneo

CECIL ODONGO: Teuzi za Rais Ruto za Makatibu wa Wizara hazikuzingatia usawa wa kimaeneo

NA CECIL ODONGO

RAIS William Ruto mnamo Jumatano alitoa orodha ya watu 51 ambao watapigwa msasa na kamati mbalimbali za Bunge la Kitaifa ili kuwa Makatibu wa Wizara.

Kilichojitokeza katika orodha hiyo ni kwamba hakuna usawa wa uwakilishi wa kimaeneo.

Zaidi ya nusu ya walioteuliwa wanatoka ngome za Kenya Kwanza za Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

Maeneo mengine ni kama yalipokezwa makombo, pengine kutokana na miegemeo yao ya kisiasa na jinsi yalivyopiga kura katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Eneo la Nyanza ambalo ni ngome ya kisiasa ya kinara wa muungano wa Azimio, Raila Odinga, lilipewa nafasi mbili za makatibu hao.

Raymond Omollo kutoka Homa Bay amependekezwa kuwa Katibu wa Usalama na Utawala huku Alfred K’Ombudo kutoka Nyakach, Kisumu, akipendekezwa kuhudumu kama Katibu wa Biashara.

Kwa jumla kaunti za Nyanza sasa zina mawaziri wawili – Waziri Eliud Owalo wa Teknolojia na Mawasiliano akiwakilisha Luo Nyanza na Ezekiel Machogu wa Elimu akiwakilisha Abagussi – pamoja na makatibu hao wawili iwapo wataidhinishwa.

Kenya ni taifa moja na umoja huo unastahili kuwa dhahiri katika teuzi anazofanya Rais.

Ni muhimu kwamba teuzi za maafisa wakuu serikalini – mawaziri, makatibu, mabalozi, wakuu wa mashirika ya serikali (parastatals) – zifanyike bila kuonekana kutenga au kuadhibu maeneo ambayo yaliunga mkono upinzani katika uchaguzi.

Watu kutoka maeneo ambayo sasa yanaonekana yametengwa na utawala wa Kenya Kwanza, pia ni walipa ushuru nchini.

Kando na kupokea huduma, uwakilishi sawa wa kimaeneo katika serikali ni hitaji la Katiba yetu.

Huu mtindo wa jamii iliyounga mkono upinzani kutowakilishwa ama kupewa makombo kwenye serikali ikome iwapo tunataka kukuza na kuwa taifa lenye umoja.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa kamishna wa ardhi ashtakiwa kwa njama ya kuuza...

UN, Amerika zasifu Ethiopia kwa kusitisha vita na Tigray

T L