• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Ashangaza kuambia korti bangi humpa motisha kulima shambani  

Ashangaza kuambia korti bangi humpa motisha kulima shambani  

NA TITUS OMINDE

MWANAMUME aliyepatikana na bangi Eldoret, alishangaza korti akijitetea kuwa ‘dawa’ hiyo haramu ya kulevya humpa motisha kulima shambani. 

Dismas Sasiya, 24 alitiwa nguvuni mnamo Julai 10, 2023 akiwa na misokoto 50 ya bangi.

Jamaa huyo alikamatwa akiwa katika kituo cha kibiashara cha Naiberi, Kaunti Ndogo ya Ainabkoi, Eldoret.

Alipofikishwa mahakamani, alishtua watu akidai bangi alishikwa nayo haikuwa ya kuuza “bali ni ya kuvuta inipe nguvu kulima shambani”.

Polisi walidai kuwa mshtakiwa ni muuzaji sugu wa bangi mtaani humo baada ya kupatikana na bangi hiyo yenye thamani ya Sh2, 500.

Hata hivyo, Bw Sasiya alikana madai ya kuwa muuzaji wa bangi ila alikubali kuwa bangi ambayo alipatikana nayo ilikuwa kama dawa ambayo anatumia ili kupata nguvu za kulima mashamba mtaani mwao.

“Ni kweli nilipatikana na bangi hii lakini madai ya kuwa muuzaji si ya ukweli. Ukweli ni kwamba mimi hutumia bangi hii kama dawa ya kuniongezea nguvu za kulimia watu mashamba ili nipate mkate wa kila siku,” alikiri mbele ya Hakimu Mkuu Denis Mikoyani.

Kijana huyo alisababisha kicheko mahakamani aliposema kwa siku yeye hutumia misokoto kumi, hivyo basi misokoto hiyo ilikuwa kipimo cha siku tano za kufanya kazi ya kulima mashamba.

Mahakama ilimhukumu kifungo cha miezi sita gerezani au kulipa faini ya Sh20, 000.

“Kwa vile mwenyewe umekiri shtaka la kupatikana na bangi kinyume cha sheria, mahakama hii imekuhukumu kifungo cha miezi sita gerezani au ulipe faini ya Sh20,000,” Hakimu aliamuru.

Hayo yakijiri, katika mahakama hiyohiyo mwanamke mmoja alikana mashtaka ya kupatikana akipanda bangi shambani mwake, katika Kaunti Ndogo ya Turbo.

Mashtaka yalisema kuwa Gentrine Andayi alipatikanaa akiwa amepanda mashina matatu ya bangi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya kudhibiti dawa ya kulevya.

Maelezo ya mashtaka yalisema kuwa mshtakiwa alipatikana akipalilia mmea huo mnamo Julai 10, 2023.

Hata hivyo, alikana mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100, 000 au pesa taslimu Sh60,000.

Kesi hiyo itatajwa Julai 31, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Wanaume Makutano-Mwea walia kuporwa na makahaba wakiponda...

Julai 16: Waziri Kindiki aadhimisha siku maalum ya kuzaliwa

T L