• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Wanaume Makutano-Mwea walia kuporwa na makahaba wakiponda raha

Wanaume Makutano-Mwea walia kuporwa na makahaba wakiponda raha

NA MWANGI MUIRURI  

VISA vya wanaume wanaosaka huduma za ngono kuporwa na kuachwa wakiwa hoi na makahaba Mji wa Makutano ulioko mpakani mwa Kaunti za Kirinyaga na Embu, vimeandikisha kuongezeka waathiriwa wakiiomba serikali kuingilia kati kuwaokoa.

Aidha, wanaume walio na pesa kufungiwa katika madanguro ya ukahaba wakiporwa ni baadhi ya changamoto za wateja wa mahaba katika mji huo.

“Tuko katika hali mbaya hapa Makutano kwa kuwa kila kuchao kilio ni wanaume kuporwa pesa mifukoni, kwa mikoba na hata kwa akaunti za benki na simu,” akasema mmoja wa wanaume walioongea na Taifa Leo Dijitali.

Alisema kwamba “licha ya udhaifu na unyonge wao wana haki kubakia salama kama binadamu mwingine yeyote…hata kama biashara ya ukahaba ni haramu”.

Walifungua roho kufuatia kisa ambapo makahaba wawili wanaodaiwa kupora mwanamume Sh107,000 walikamatwa katika mji huo, lakini wakaachiliwa katika hali ya isiyoeleweka.

Kukamatwa kwa wawili hao kulitandaza hali ya taharuki miongoni mwa makahaba mjini humo, ambapo baadhi walio na kashfa za uporaji walionekana kusafiri kuhepa msako huo.

Wanawake hao wawili walidaiwa kuwa walitekeleza wizi huo mnamo Juni 30, 2023 kupitia simu ya mkono ya mwanamume mlalamishi.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Mwea Bi Jane Manene, biashara ya ukahaba ni haramu.

“Lakini kuna wale wanawake na wanaume ambao hujiingiza katika mikataba ya kuelewana kimapenzi…Hiyo ni sawa bora kusiwe na ushirika wa watoto. Lakini pia, kuibiana pesa na vitu vingine vya thamani ni kinyume na sheria,” akasema.

Aliwahimiza wanaume walio na mazoea ya kutembea katika maeneo hatari kama hayo ya Makutano wawe wakichukua tahadhari kuu kuhusu mali yao.

“Tungetaka wanaume waturahisishie kazi kupitia kukinga pini zao za akaunti dhidi ya wakora na pia kujua usalama wao ni jukumu lao wenyewe. Tunafaa kukabiliana na visa hatari vya uhalifu nao raia wakitusaidia kuzima ukora wa viwango vya chini kupitia kuchukua tahadhari,” akasema.

 

  • Tags

You can share this post!

Mbunge Kwenya Thuku adai ufugaji ng’ombe Nyandarua ni...

Ashangaza kuambia korti bangi humpa motisha kulima shambani...

T L