• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 9:49 AM
Atwoli aunga mkono hatua ya Sakaja kuondoa matatu CBD Nairobi

Atwoli aunga mkono hatua ya Sakaja kuondoa matatu CBD Nairobi

NA SAMMY WAWERU

KATIBU Mkuu Muungano wa Kutetea Wafanyakazi Nchini (Cotu), Francis Atwoli ameunga mkono tangazo la Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja kuondoa matatu katika kitovu cha jiji.

Kauli ya Bw Sakaja imekosolewa na wahudumu wa matatu, Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua akiwapiga jeki.

Kulingana na Bw Atwoli, hatua ya Gavana Sakaja itasaidia kuleta hadhi ya jiji la Nairobi.

“Tunataka waunge mkono Bw Sakaja, tunataka Nairobi ionekane kama miji mingine safi,” akasema Katibu huyo.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Agosti 9 Atwoli alikuwa akiunga mkono kuchaguliwa kwa kinara wa Azimio la Umoja One Kenya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, na mwishoni mwa 2022 alionekana kubadilisha msimamo wake na kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt William Ruto.

“Nairobi isiwe jiji ambalo watu wa matatu wamejaa ndani, watu wa bangi wamejaa…Iwe kama miji mingine ya kimataifa kama vile Abuja (Nigeria), Cairo (Misri), Johannesburg (Afrika Kusini), Harare (Zimbabwe) na Kigali mji mchanga mno Rwanda,” Bw Atwoli akaelezea.

“Turejeshe hadhi ya Nairobi kwa kuunga mkono pendekezo la Gavana Sakaja na tutakuwa na huduma za uchukuzi zenye mpangilio bora,” akaongeza.

Chini ya serikali ya Jubilee iliyoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na naibu wake Ruto (ambaye kwa sasa ni Rais), aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alizindua mpango wa mabasi maalum (BRT) kufanikisha shughuli za uchukuzi Nairobi, mkakati ambao kufikia sasa haujawahi kutekelezwa.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona na Espanyol nguvu sawa katika mechi ya La Liga...

Viongozi wa ODM Pwani waunga serikali ya Ruto

T L