• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:54 PM
Baba azuiliwa kwa siku 14 uchunguzi wa mauaji ya mwanawe ukiendelea

Baba azuiliwa kwa siku 14 uchunguzi wa mauaji ya mwanawe ukiendelea

NA TITUS OMINDE

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 54 anayeshukiwa kumuadhibu hadi kufa mwanawe wa kiume aliyekuwa amelewa, amezuiliwa kwa siku 14 hadi uchunguzi wa mauaji hayo utakapokamilika.

Mahakama ya Eldoret mnamo Jumanne imewaruhusu maafisa wa upelelezi kutoka kituo cha polisi cha Baharini kumzuilia Paul Rugut baada ya afisa mpelelezi Nicholas Ndalo kuambia mahakama kuwa kutokana na utata wa suala hilo alitaka muda zaidi wa kumhoji mshukiwa kuhusiana na kesi ya mauaji.

Bw Ndalo alimweleza Hakimu Mwandamizi Onkoba Mogire kwamba kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Baharini na chifu wa eneo la Kapyemit, Philemon Birech.

Kulingana na polisi, mwili wa Vincent Kimutai,22, ambaye alifuzu hivi maajuzi kwa shahada ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Eldoret ulipatikana karibu na eneo la Green Hills karibu na Sirikwa Quarry mnamo Agosti 21, 2023.

Mahakama iliambiwa kuwa siku iliyotangulia, marehemu alikuwa mlevi na mwenye jeuri ambapo baba yake alimwadhibu kwa kufanya vurugu na ukaidi.

Inadaiwa ni baada ya kichapo hicho ambapo mwili huo ulipatikana umetupwa eneo hilo la Sirikwa.

Polisi walimkamata mzazi huyo kama mshukiwa mkuu kwa vile familia ilikuwa haijaripoti kwamba kulikuwa na mtu aliyepotea hadi mwili ulipogunduliwa ukiwa pahala hapo.

Mwili huo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret na maafisa wa polisi waliozuru eneo la mkasa.

Akitoa ombi la kuzuiliwa kwa mshukiwa huyo, afisa mpelelezi aliiambia mahakama kuwa bado hajaandikisha taarifa kutoka kwa mashahidi wakuu ambao ni wa kutoka katika familia ya marehemu.

Aidha aliambia mahakama kuwa mshukiwa mkuu ni baba wa marehemu na iwapo ataachiliwa kwa dhamana, kuna uwezekano wa kuingilia upelelezi.

Mahakama iliwaruhusu maafisa wa upelelezi kumzuilia mshukiwa huyo kwa siku 14 hadi uchunguzi ukamilike.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 11, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Firat motoni kwa kupuuza wachezaji wa Gor, Tusker na Ingwe...

Waasi wa ODM Nyanza wataka wakazi wamteme Raila

T L