• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
BAT ByPass Thika kukamilika katika muda wa wiki chache zijazo

BAT ByPass Thika kukamilika katika muda wa wiki chache zijazo

Na LAWRENCE ONGARO

MSONGAMANO wa magari utapungua pakubwa barabara ya BAT Bypass itakapokamilika baada ya miezi minne ijayo.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina na mwenzake wa Gatanga Bw Nduati Ngugi walizuru eneo la Delmonte ambako barabara ya umbali wa kilomita 15 ya BAT Bypass itapitia.

Bw Wainaina alisema kwa muda mrefu kumekuwa kukishuhudiwa msongamano wa magari yanayoingia Thika kutoka Nairobi na hata upande wa Murang’a.

“Iwapo barabara hiyo ya kuingia Delmote na kutokea eneo la BAT itakamilika, bila shaka msongamano wa magari utapungua. Huu pia ni mwamko mpya katika usafiri na biashara,” alisema Bw Wainaina.

Alisema kampuni ya Delmonte ambayo imeajiri wafanyakazi 7,000 itapata nafasi ya kusafirisha mananasi na bidhaa nyinginezo katika maeneo tofauti kama Murang’a, Machakos, na hata Nyandarua.

Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliwashauri wakazi wa Umoja ambako barabara hiyo itapitia wajipange mapema na kuhama kabla hawajabomolewa nyumba zao. Aliwataka wajipange mapema ili wasije wakashtuliwa bila kutarajia.

Kulingana na mhandisi wa mradi huo, barabara hiyo itagharimu takribani Sh1.8 bilioni kabla ya kukamilika.

Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi ambaye barabara hiyo ya BAT Bypass inapitia katika eneo lake alipongeza mradi huo akisema biashara itaimarika pakubwa ambapo bidhaa zitasafirishwa haraka bila kuchelewa.

Wakazi wa Ithanga watapata nafasi nzuri ya kusafirisha bidhaa zao huku wakazi wa Murang’a nao wakipata fursa ya kusafirisha ndizi kwa wingi katika maeneo mengine,” alisema Bw Ngugi.

Alisema wakazi wa Murang’a watasafiri kwa urahisi kufika Thika, Nairobi, hadi kwenda sehemu za Ithanga.

Kwa muda mrefu wafanyabiashara wengi wa Murang’a wamepati wakati mgumu kusafirisha bidhaa zao kwa sababu ya ubovu wa barabara, kulingana na Bw Ngugi.

Aliwataka wakazi wawe mstari wa mbele kushirikiana na wahandisi hao.

Mhudumu wa bodaboda kutoka eneo la Delmonte Bw Stephen Kimilu alisifu mradi huo wa barabara akisema utawasaidia kuendesha kazi yao kikamilifu.

“Hapo awali tulipata shida hasa wakati wa mvua kwa sababu matope yalikuwa tele katika barabara ya kuingia kampuni ya Delmonte. Sasa tutapata afueni ikikamilika,” alisema Bw Kimilu.

Naye dereva wa lori la mizigo Bw Francis Wanyoike alisema itakuwa afueni kwa ujenzi wa barabara hiyo baada ya kutaabika muda mrefu.

“Sisi kama madereva tunastahili kupongeza juhudi hizo kwa sababu bidhaa zitasafirishwa kwa wakati ufaao,” alisema Bw Wanyoike

You can share this post!

LISHE: Sukumawiki na nyama ya mbuzi

AC Milan wamsajili fowadi matata raia wa Croatia, Mario...