• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Bei ya unga kupanda wakulima wakikwamilia mahindi

Bei ya unga kupanda wakulima wakikwamilia mahindi

Na GERALD ANDAE

BEI ya unga wa mahindi inatarajiwa kupanda baada ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), kuongeza bei ya mahindi kwa Sh300 kutoka Sh2,700 hadi Sh3,000 kwa gunia la kilo 90.

Bei hiyo mpya italazimisha kampuni za kusaga unga wa mahindi kuongeza bei ya kununua zao hilo kutoka kwa wakulima ili zipate mahindi ya kutosha.

Ongezeko la bei ya mahindi ambayo ni asilimia 80 ya gharama yote ya usagaji wa unga, litafanya bei kuongezeka zaidi kutoka Sh100 kwa pakiti ya kilo mbili.

NCPB inasema bei hiyo mpya itawezesha wakulima kupata thamani ya mahindi wanayoiuzia.

“Bei ya Sh3,000 tunayotoa itafanya wakulima kupata thamani ya mahindi wanayotuuzia,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NCPB , Bw Joseph Kimote.

Kwa wakati huu, wafanyabiashara wananunua gunia mola la kilo 90 la mahindi kwa Sh3,000 kutoka kwa wakulima ikiwa bei ya juu zaidi katika miaka mitatu iliyopita.

Tayari kampuni za kusaga unga zimelalamikia bei ya juu ya mahindi huku kukiwa na uhaba wa zao hilo kwa kuwa wakulima hawauzi mahindi yao wakitarajia bei nzuri miezi ijayo.

Wiki moja iliyopita, kampuni hizo ziliandikia barua waziri wa kilimo Peter Munya kuonya kuhusu kupanda kwa bei ya unga kutokana na bei ya juu ya mahindi nchini.

Bw Kimote alisema wakulima watakuwa wakilipwa saa 24 baada ya kuwasilisha mahindi katika depo za NCPB.

“Hakuna masharti ya usimamizi ya mtu kuwasilisha mahindi yake kwa bodi mradi yatimize viwango vya ubora vya Shirika la Ukadiriaji Ubora wa bidhaa la Kenya,” alisema.

Alisema kwamba bodi pia inahifadhia wakulima zao lao, huduma za kukausha nafaka, kusafisha na kupima viwango vya sumu ya kuvu.

You can share this post!

Wawekezaji walilia Balala aokoe utalii

Lamu yaongoza kwa ajali za mashua baharini – ripoti

T L