• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Familia yataka maswali yajibiwe kuhusu mauaji ya jamaa yao

Familia yataka maswali yajibiwe kuhusu mauaji ya jamaa yao

NA WYCLIFFE NYABERI

Familia moja kijijini Ibacho, eneobunge la Nyaribari Masaba kaunti ya Kisii ingali inatatizika na kifo cha mpendwa wao aliyeuawa mwaka mmoja uliopita.

Caleb Monyenye, aliachwa na majeraha mabaya ya mapanga kichwani na watu wasiojulikana mnamo Juni 19, 2022.

Jamaa zake walimpata asubuhi ya siku hiyo akiwa hajifahamu katika soko la Ibacho na kumkimbiza hospitalini.

Kwa bahati mbaya, alifariki baada ya mwezi mmoja katika Hospitali Kuu ya Kenyatta.

Kutokana na utata uliozingira kifo chake, maafisa kutoka kitengo cha upelelezi (DCI) walifika kijijini humo kuanzisha uchunguzi wa kifo cha Monyenye.

Lakini hadi sasa, hawajapata majibu kuhusu kifo cha mpendwa wao na sasa wanaiomba serikali kuwapa ripoti ya uchunguzi walioufanya.

“Tunataka kujua ni kina nani waliomuua ndugu yetu. Hatujapata ripoti kamili kutoka kwa DCI mwaka mmoja sasa. Ndio maana tunalia tukiomba tufahamishwe yale yaliyotendeka,” akasema Bi Dinah Monyenye, dada mkubwa wa marehemu.

Collins Otundo, mwanawe marehemu aliambia Taifa Dijitali kuwa baba yao alikuwa mtu aliyependa kutangamana na watu wote.

“Hakuwa na kinyongo na mtu yeyote. Baba alikuwa mtu wa hulka nzuri na hadi kufikia sasa hatuelewi ni kwa nini alipigwa vile. Alikuwa mtu aliyeipenda familia yake,” Bw Otundo aliongeza.

Paul Monyenye, ndugu mkubwa wa mwendazake naye aliungana na wenzake kuiomba serikali iwafahamishe matukio yaliyopelekea ndugu yao kuuawa.

“Tunamwomba Rais William Ruto na waziri wake wa Ulinzi Profesa Kithure Kindiki kuingilia kati. Tumekwisha kubali alifariki na hatarudi lakini ni vyema kujua ukweli. Pia tunatumai habari hii itamfikia mkuu wa DCI Amin Mohamed ili atusaidie,” ndugu huyo alieleza.

  • Tags

You can share this post!

Mume na mkewe katika kesi ya unyakuzi wa ardhi Lavington...

Mkituruhusu kuchukua ranchi ya Giriama, tutamaliza tatizo...

T L