• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Gavana Ndeti abubujikwa na machozi kuona waathiriwa wa ubomozi Portland wakihangaika

Gavana Ndeti abubujikwa na machozi kuona waathiriwa wa ubomozi Portland wakihangaika

NA FRIDAH OKACHI

GAVANA wa Machakos Wavinya Ndeti amemkosoa Rais William Ruto kwa kupuuza ombi lake kusitisha ubomoaji unaoendelea kwenye ardhi yenye utata ya East African Portland Cement, mahangaiko wanayopitia waliofurushwa yakimchochea kububujikwa na machozi.

Bi Wavinya alisema Rais Ruto aliahidi kutatua mzozo wa shamba hilo, kabla kusafiri China.

Kiongozi wa nchi alienda China mnamo Oktoba 14, 2023 kwa ziara ya kikazi, safari inayosemekana pia anatarajiwa kuomba mkopo zaidi kutekeleza miradi ya maendeleo Kenya.

“Mbona unatufanyia hivi Rais, Mheshimiwa Ruto ingekuwa kwako, ungekubali ifanyike? Hatutaruhusu uendelee kubomoa nyumba na makanisa,” Gavana Ndeti alisema, huku akionekana kulemewa na machozi.

Aidha, alilaani vikali hatua ya Kampuni ya East African Portland Cement (EAPCL), kwa kubomoa nyumba za wakazi pamoja na makanisa matano, na shule tatu.

Bi Wavinya amemsuta Dkt Ruto kwa kutumia maafisa wa polisi kulinda oparesheni aliyotaja kuwa haramu, wakazi wakiachwa hoi bila makao.

“Niliongea na Rais na akasema ataangalia. Hivi sasa, watu wetu wanafukuzwa, uharibifu wa mali isiyomithilika umefanyika. Sasa hivi mvua ya El Nino inatarajiwa na mtihani utaanza hivi karibuni. Walioathirika wataenda wapi?” Gavana Wavinya akataka kujua.

Hii ni mara ya pili ubomoaji kufanyika katika ardhi hiyo yenye utata, Serikali ya Kaunti ya Machakos ikijiondolea lawama.

Gavana Wavinya ametishia kuenda mahakamani kutafuta suluhu.

“Hili ni shamba la watu binafsi, wala si la serikali,” alisisistiza.

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka pia amezuru shamba hilo akimrai Rais Ruto kukomesha ubomozi unaondelea.

Utata wa shamba hilo la Hekta 4, 298, ulianza kutokota 2016.

Kampuni ya East African Portland Cement iliweka bango la ilani, ikionya watu dhidi ya kununua vipande vya ploti.

 

  • Tags

You can share this post!

Polisi aliyeua mumewe kuzuiliwa kwa siku 14 uchunguzi...

Wawili wafariki ubomoaji ukichacha mjini Mavoko

T L