• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Wawili wafariki ubomoaji ukichacha mjini Mavoko

Wawili wafariki ubomoaji ukichacha mjini Mavoko

NA STANLEY NGOTHO

HALI ya taharuki iliendelea kutanda jana katika eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos, baada ya waathiriwa wawili wa ubomoaji unaoendelea kufariki, shughuli hiyo ikiingia siku ya nne leo.

Ubomoaji huo unahusu ardhi yenye utata, inayodaiwa kumilikiwa na kampuni ya kutengeneza saruji ya East African Portlands Cement (EAPC).

Mmoja wa waathiriwa hao (wote ni wanaume), anayedaiwa kujenga nyumba ya kukodisha yenye thamani ya mamilioni ya pesa, aliripotiwa kuzimia nyumbani kwake jijini Nairobi na kufariki.

Ripoti zilieleza kuwa mwanamume huyo alifariki baada ya kufahamishwa kwamba nyumba yake ilibomolewa Jumapili asubuhi.

Mwathiriwa wa pili anadaiwa kufariki baada ya kujitia kitanzi Ijumaa usiku baada ya nyumba yake ya kifahari kubomolewa.

“Inasikitisha kuwa jamaa yetu alizidiwa na habari hizo za kubomolewa nyumba yake. Alijitoa uhai jana (Jumapili) usiku,” akasema jamaa ya mwathiriwa huyo ambaye hakutaka kutajwa.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Athi River, Bw Jos Mudavadi, aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba tukio hilo bado halijaripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Athi River.

“Hatuwezi kupuuza suala hilo japo hakuna ripoti yoyote rasmi iliyowasilishwa kwetu. Kwa sasa, huo ni uvumi tu. Ikiwa matukio kama hayo yatafanyika, nazishauri familia zitakazoathiriwa kuripoti kwetu ambapo tutafuatilia,” akasema.

Hapo jana, ubomozi huo wa makazi ya kifahari, makanisa na shule uliingia katika siku ya tatu.

Ubomoaji huo uliendeshwa na matingatinga ya serikali na watu binafsi, yaliyobomoa majengo hayo bila huruma.

Sauti ya matingatinga hayo ilisikika kote kote, huku eneo nzima likijaa vumbi lililotoka kwa majengo yaliyobomolewa.

Zaidi ya nusu ya ardhi hiyo yenye utata yenye ukubwa wa ekari 4, 268 ilikuwa imegeuzwa mahame.

Waathiriwa walijaribu wawezavyo kuokoa chochote ambacho wangeweza kabla majengo yao kufikiwa na matingatinga hayo.

Watu kadhaa walikamatwa na polisi wakiiba vifaa vya majengo hayo. Biashara ya uuzaji vyuma ilinoga huku wezi wakilenga majumba makubwa ya kifahari.

Bw Zacharia Marwa, 53, aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba alipoteza biashara yenye thamani ya Sh4.5 milioni.

Alikuwa amechukua mkopo kujenga nyumba tatu za kukodisha.

“Nilinunua ploti mbili kutoka kwa chama cha ushirika kwa Sh400,000 kila moja, miaka mitano iliyopita. Nina vyeti rasmi kuonyesha umiliki wake. Kwa sasa, nyumba hizo zimebaki vifusi tu, baada ya kubomolewa,” akasema.

Bi Eunice Wanjugu alisema alikuwa ametumia Sh18 milioni kujenga nyumba za kisasa kama makazi yake ya uzeeni. Akibubujikwa na machozi, Bi Wanjugu aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba alikuwa amekopa Sh2 milioni kutoka kwa benki ili kuongeza fedha za kujengea makazi yake.

“Tunairai serikali kutulipa fidia kutokana na hasara tuliyopata. Sidhani kama nitawahi kusahau tukio hili. Ujenzi wa makazi yangu ulikuwa umekaribia kukamilika. Sasa yamebaki kuwa vifusi tu,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Ndeti abubujikwa na machozi kuona waathiriwa wa...

Huyu rafiki ataniambukiza tabia za usagaji?

T L