• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Gretsa yatenga Sh100 milioni za upanuzi wa chuo

Gretsa yatenga Sh100 milioni za upanuzi wa chuo

Na LAWRENCE ONGARO

WAHITIMU wapatao 667 wa Chuo Kikuu cha Gretsa mjini Thika, wameshauriwa kutumia ujuzi walio nao bila kupoteza fursa zilizoko katika soko la ajira.

Chansela wa chuo hicho Dkt Kibathi Mbugua, alisema kuwa licha ya kupitia masaibu mengi wakati wa janga la Covid-19, wahadhiri na wanafunzi wa chuo hicho walijitahidi na kuafikia matakwa yao katika elimu.

“Wakati nchi ilikuwa imekabiliwa vilivyo na janga la Covid-19 mambo yalikuwa magumu kwa sababu masomo mengi yalifuatiliwa kupitia mitandao huku wanafunzi wakiwa wachache madarasani,” alifafanua Dkt Mbugua.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi, katika awamu ya 12 ya kufuzu kwa wahitimu katika chuo hicho.

Alisema wamekuwa na tatizo la ukosefu wa mahali pa malazi kwa wanafunzi na hilo limefanya watafute kipande cha ardhi cha ekari 60 eneo la Makuyu, Kaunti ya Murang’a, ili kuongeza mijengo ya kisasa.

“Tayari tumekamilisha majumba mawili yenye maktaba, madarasa kadha na jikoni. Tunafanya mipango kuona ya kwamba tunavuta maji safi na umeme katika eneo hilo,” akasema.

Alikadiria bajeti ya kukamilisha mradi huo ni takribani Sh100 milioni ili kupatikane majumba ya kisasa ya wanafunzi na wahadhiri.

Wahitimu wa Gretsa. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alitoa wito kwa serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaokamilisha masomo vyuoni ili waweze kubuni ajira zao wenyewe.

“Wanafunzi wengi wana ujuzi mwingi ambao unaweza kuwainua kimaisha iwapo watapata usaidizi wa kifedha,” alieleza Dkt Mbugua.

Naibu Chansela wa chuo hicho, Profesa Wabuke Bibi, alisema katika chuo hicho wanazingatia maswala ya utafiti na ubunifu ili kuwapa wanafunzi fursa ya kujiendeleza zaidi.

Alisema wamegundua ya kwamba masomo ya darasani pekee hayana ukamilifu bila kufanya utafiti kwa jambo fulani.

“Tunataka kuona wanafunzi kutoka chuoni wakijumuika na wananchi na kuendesha utafiti wao kuhusu maswala ya kibiashara wanayopitia. Tungetaka kuelewa mengi kuhusu hali ya mashinani,” alifafanua Prof Bibi.

Alipongeza wahadhiri wa chuo hicho kwa kukubali kukatwa mishahara kiasi fulani hasa wakati wa janga la Covid-19.

“Wakati huo mambo yalikuwa magumu na tuliendesha mipango yetu jinsi mambo yalivyokuwa. Hata wakati mwingi wahadhiri na wanafunzi wengi wakiendesha shughuli zao za kimasomo wakiwa nyumbani,” alieleza Prof Bibi.

Alikubaliana na maono ya Dkt Mbugua ya serikali kuwapiga jeki kifedha wanafunzi baada ya kukamilisha masomo yao.

“Ni jambo la kuvunja moyo wakati mwanafunzi anasoma kwa miaka minne halafu baada ya kukamilisha elimu yake anaketi bure nyumbani bila kufanya lolote,” alieleza msomi huyo.

Alieleza wanafunzi wanastahili kupewa motisha ili masomo yao chuoni yawe na maana badala ya kuketi bure wakingoja kupata ajira.

You can share this post!

Man-United waripoti visa vingi zaidi vya corona

Argentina na Italia kuchezea gozi la Finalissima jijini...

T L