• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Huenda chama cha Knut kikashindwa kuinuka tena

Huenda chama cha Knut kikashindwa kuinuka tena

Ngumi ya tumboni ambayo Chama Cha Kuajiri Walimu nchini (TSC) kiligonga Chama Cha Kutetea Maslahi ya Walimu (KNUT) ilikuwa nzito sana hivi kwamba KNUT ingali inagaragara chini na itachukua muda mrefu kuinuka.

Mashindano ya ni nani bingwa kati ya KNUT na TSC yamekuwa yakiendelea kwa muda KNUT ikiongozwa na aliyekuwa katibu wake Wilson Sossion nayo TSC ikiongozwa na Bi. Nancy Macharia ambaye anaelekea kuondoka katika uongozi wa TSC.

TSC imekuwa ikisisitiza kuwa Wilson Sossion hafai kuwa akiendelea kushikilia wadhifa wa Katibu wa KNUT huku akiwa mbunge, hivyo basi ikamtaka ajiuzulu uongozini wa KNUT.Katika kuthibitisha makali yake, TSC ilianza kwa kumwondoa Bwana Sossion katika rejista ya walimu.

Hivi ni kusema kuwa Sossion hakutambuliwa tena kama mwalimu hivyo basi hana uwezo wa kuongoza walimu tena. Kana kwamba hayo hayakutosha, TSC iliunda mbinu ya kuhakikisha kuwa walimu wanajiondoa chamani kwa kuwawekea vikwazo vya kutowapandisha vyeo miongoni mwa vingine. Hili liliwapata walimu zaidi ya asilimia 70 wakikihama chama cha walimu KNUT.

Kuondoka huko kwa walimu chamani kulisambaratisha KNUT pakubwa. KNUT ikakosa fedha nyingi za utendakazi ambazo ilikuwa ikipata kutoka kwa walimu na usimamizi wake ukaanza kuingia doa.Aidha mpango wa kuwapandisha walimu vyeo na nyongeza za mishahara ya walimu limekuwa ni suala sugu ambalo limekuwa likisababisha mvutano mkali katika makundi haya.

Sossion amekuwa akionekana kusukumiza suala la kupandishwa vyeo kwa walimu kwa njia ambayo TSC haikupenda. Licha ya kuwa KNUT ina wajibu wa kutetea walimu ambao ni wateja wake, TSC ndiyo hushughulikia kupandishwa ngazi kwa walimu kwa kuwa ndiyo mwajiri wa walimu na ndiyo hukagua utendakazi wa walimu na kujua ni nani anafaa kupandishwa ngazi na ni nani ambaye hafai.

Kwa asilimia kubwa, Sossion alichangia kuporomoka kwa KNUT alipokuwa katibu wake mkuu. Shughuli za kuwapandisha vyeo walimu ni mpango wenye utaratibu maalum unaofaa kufuatwa na mwajiri kama inavyofanyika katika sekta nyingine za serikali.

KNUT inaweza tu kushinikiza TSC ifanye hivyo kwa kujadiliana na kuelewana bali si kulazimisha TSC kwa kutumia migomo na kudhalilisha masomo ya wanafunzi. Mgomo mrefu sana wa walimu wa siku 36 alioongoza Bwana Sossion bila shaka haukufurahisha serikali, wazazi na hata wanafunzi waliopotezewa muda wao.

Kulingana na Sossion, kwake mgomo huo ulikuwa ni ufanisi mkubwa. Hii ina maana kuwa KNUT haijali kamwe mahitaji ya wanafunzi kupata elimu bali haja yake ni pesa inazotoza walimu ambao ni wanachama wake. Basi hapo TSC ikaamua kukiporomosha chama hicho, ambacho kuinuka kwake tena si kazi rahisi!

  • Tags

You can share this post!

Wadau wa Pwani wataka Ligi Kuu ya Drafu ianze nchini

Corona hatari sana yaja hata kwa waliopata chanjo –...