• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Wadau wa Pwani wataka Ligi Kuu ya Drafu ianze nchini

Wadau wa Pwani wataka Ligi Kuu ya Drafu ianze nchini

KAMA ilivyo katika soka, mchezo wa drafu umeondokea kuzuzua wengi jimbo la Pwani hasa kutokana na inavyoutia idadi kubwa mashabiki kila unapochezwa.

Maeneo kama Majengo King’orani, Makande, Changamwe, Bombolulu, Kongowea, Shanzu, Mtwapa ni baadhi tu ya maeneo ambayo mchezo huu huvutia halaiki.Juhudi za kuipigia debe mchezo huu ili kuweza kuorodhoshwa kati ya michezo inayotambulika nchini zimeng’oa nanga huku wengi wakipigania kuanzishwa kwa Ligi ya kitaifa itakayoshirikisha timu kutoka kila pembe ya taifa.

John Ochare Ongere ambaye ni bingwa wa mashindano ya drafu ya Sarova Hotels Cup mwaka wa 1999, anakiri wakati umewadia kuanzishwa kwa ligi kuu ya mchezo huu nchini kama njia mojawapo ya kuvumisha zaidi mchezo unaozidi kupendwa na wengi kila uchao.

Majuzi klabu ya Majaoni Draft iliyoko Bamburi, Kisauni, Mombasa iliandaa kinyang’anyiro cha kukata na shoka ya kuweza kuwatambua wachezaji wake mahiri watakaoshiriki kinyang’anyiro cha kusaka bingwa wa wadi ya Bamburi na eneobunge nzima la Kisauni.Ni mchuano uliofaulu kuleta pamoja wachezaji mahiri kutoka wadi ya Bamburi walioweza kuonesha weledi wao wa kusukuma kete kwa ustadi.

Kati ya wachezaji watajika wa drafu jimbo la Pwani waliojikakamua na hatimaye kufika kushuhudia mtanange huu ni bingwa wa Maimuna Salim Cup Omar Madushi, Alex Wafula kutoka klabu ya Shanzu Draft na Saafri Ngalla anayetamba sana maeneo ya Kisauni.Hata hivyo, ulipowadia wakati wa kuonesha ubabe, George Ngala alijikuta akijikuna kichwa bila kupata suluhu aliposhindwa na Safari Ngala kwa alama 6-0 huku John Ponda akitumia wembe huo huo kumnyoa Albert Wanje kwa alama 6-0.

Pandao Tsuma naye akajidhihirisha kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kumshinda Sammy Nyenyo kwa alama 2-1 katika pambano kali lililoshangiliwa na mashabiki kwelikweli.Wengine waliotamba katika michuano yao ni Francis Kaloki aliyemshinda Festus Karisa kwa alama 2-1 naye Sultan Mwavua akamfunzwa namna ya kucheza na Albert Ziro aliyemduwaza kwa alama 2-1.

Aidha, baada ya mgaragazano wa siku tatu uliyowezesha kila mshiriki kujitupa ugani mara tisa hatimaye mbivu na mbichi ikabainika.Safari Ngalla aliibuka kidedea katika chati akizoa jumla ya alama 56 akifuatwa kwa karibu sana na John Ponda kwa alama 52, nafasi ya tatu ikinyanyuliwa na Francis Kaloki kwa alama 46.

Wengie walioonesha umahiri katika michauno yao ni Katana Festus na Pandao Tsama kila mmoja akifaulu kupata alama 42. Sammy Nyenyo akiridhika na nafasi ya sita kwa alama 38 akifuatwa na Safari Kombe kwa alama 35.

Albert Wanje alimaliza wa nane kwa alama 30, Peter Ngalla alama 29 huku George Ngalla akifunga ‘ Kumi Bora ‘ kwa alama 23.Baada ya michuano hii, msemaji wa klabu ya Majaoni Draft Club Karisa Festus Thoya aliwataja wachezaji bora kumi kuwakilisha klabu hiyo katika shindano la kumsaka bingwa wa wadi ya Bamburi mwezi ujao.

“ Wachezaji wetu wameonesha mchezo wa hali ya juu katika mashindano haya jambo ambalo limetupatia motisha ya kukabiliana na wapinzani wowote wakati wowote,” asema Thoya.Thoya alielezea Dimba kwamba kabla ya kushiriki mashindano ya kumsaka gwiji wa mchezo huu katika wadi ya Bamburi, wananuia kusafiri hadi eneoubunge la Mvita kuchuana na mibabe ya Makande wiki ijayo.

  • Tags

You can share this post!

OCS kufikishwa kortini leo kwa madai ya kuchukua hongo

Huenda chama cha Knut kikashindwa kuinuka tena