• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Iwapo ukeketaji ni dawa, basi mbona michepuko kwenye ndoa?

Iwapo ukeketaji ni dawa, basi mbona michepuko kwenye ndoa?

NA STEPHEN ODUOR

Ukeketaji ni mojawapo ya mila ambazo baadhi ya jamii katika Kaunti ya Tana River zimekuwa zikitetea mno kwa madai ya kwamba huzuia kuchepuka kwa mabinti na wanawake katika ndoa.

Igizo la jinsi waliokeketwa hufungwa miguu baada ya kukeketwa hadi watakapopona jeraha. Picha|Stephen Oduor

Baadhi ya wazee na vijana kwa ujumla wamekuwa wakishinikiza dhana ya kuwa mwanamke aliyekeketwa hawezi kuchepuka, na basi ndio wanawake shwari kwa ndoa.

Ni dhana ambayo imekita mizizi kwa miongo mengi ila sasa kitumbua kimeingia mchanga, kwani, talaka zinazidi kila uchao, huku wanandoa wakidaiwa kutokuwa waaminifu kwenye ndoa.

Ismael Hassan atakuwa anafunga ndoa yake y tatu baada ya kutoa talaka mbili kwa wake zake akidai hawakuwa waaminifu.

“Wote walikuwa wa kabila langu, mke wa kwanza tuliishi miaka tisa, tulipokosana kidogo tu, nikakuta ametoka na jirani yetu na hakukana, nikampa talaka yake. Saa hizi anaishi na yule mwenzangu ambaye ni m’bara aliyeslimu,” anasimulia.

Ndoa yake ya pili vile vile haikumaliza masaa ishirini na manne, kwani anadai kuwa mwanadada alimhadaa kuwa alikuwa na ubikra wake kamili, ila usiku wa kushiriki tendo la ndoa baada ya Nikah, alipata hali sivyo.

Kwa sababu ya hofu ya kusambaratika kwa ndoa ya kwanza, hakuwa na imani kuwa ndoa ya pili ingestahimili muda wake, hivyo aliwaita wazee na wazazi wake na kuweka mambo bayana, na hivyo akaruhusiwa kutoa talaka kwa mkewe wa pili.

“Nimekaa sasa kwa muda wa miaka mitatu manake nilipatwa na mshtuko na msongo wa mawazo, nikaamua nichunguze sana wasichana wetu nikapata kwa kweli kuna mambo ambayo hayako sawa, wamejua mengi na wanatafuta mambo mengi, sio kama enzi za wazazi wetu,” anasema.

Bw Hassan amejitafutia mke mwenye asili ya bara, mwanadada kutoka mjini Meru, akiwa na tumaini la kuwa ni bikra kama anavyodai.

Anasema kuwa hana imani tena na wanadada wa kabila lake akisema iwapo atataka kuoa bikra, basi itambidi aozwe mtoto wa shule ya msingi.

“Malezi siku hizi yamekuwa hafifu, msichana akishamaliza shule ya upili sasa shughuli yake ni kutangatanga tu, na jinsi kumekuja ugatuzi kuna pesa mitaani, wanapotelea hapo,” anasema.

Ibrahim Godana naye angali anauguza majeraha ya moyo baada ya kumkuta mkewe mchana kutwa akichepuka na mfanyakazi wake.

“Mimi nilikuwa nimesafiri kwenda kuona mifugo malishoni kwa siku kadhaa, kurudi nikawakuta waziwazi kule kwa nyumba ya kijakazi saa tisa mchana,” anasimulia.

Ilimbidi kusitisha ndoa yake ya miaka kumi na miwili na kumfukuza mkewe naye akabaki na watoto.

Analaumu vikundi vya akina mama kama chanzo cha kuwapotosha wake zao na kuwafunza kuchepuka, kwani, kabla hawajajiunga na vikundi hivyo, walikuwa watiifu na waaminifu.

“Sielewi manake mimi nimekuzwa nikijua kuwa ukeketaji ndio suluhu na kufuli ya ndoa, ila sasa inanikanganya manake sio mimi tu katika majonzi, tuko wengi, hatuwaelewi hawa wanawake wetu,” anasema kwa huzuni.

Bi Fiyan Mohammed hata hivyo anadai kuwa, wanaume katika jamii zao wamekuwa wakiwahadaa wake zao kwa muda mrefu na ndipo kuchangia matukio kama haya.

Anasema kuwa, wanawake hujitolea kukeketwa ili kuwapendeza waume zao, ila tu wanaume hao kuelekea kuchovya mabinti wa mitaani kutoka bara na kumalizia pesa zao kule.

“Mwanaume anakuacha na watoto, anaenda anauza ng’ombe ama mbuzi kisha unamwona baada ya mwezi mzima, kumbe alikuwa kwa Njeri wakiponda raha, mimi nina watoto nafaa niwalishe, nitatafuta namna kama mwanamke,” anasema.

Bi Mohammed anadai kwamba baadhi ya wanawake katika jamii zinazoshiriki ukeketaji hughafilika moyoni na mateso wanayopata kutoka kwa waume zao, na hivyo kulipiza kisasi.

Anaongezea kuwa baadhi ya waume zao humaliza nguvu katika michepuko nje ya ndoa, hivyo basi hushindwa kujukumika kwa wake zao vilivyo na kuwaacha wakiwa na kiu.

“Wakishaonja tu kwa Njeri, wanachanganyikiwa kabisa na wanaanza kuwa na dharau, hapo sasa ndipo atakwambia jinsi wewe umekeketwa na hujui hili na lile, anakuwa mwanasayansi wa mwili wako, anakufedhehesha mpaka unahisi wewe si mtu tena,” anasema kwa jazba.

Anabaini kuwa, baadhi ya wanawake waliokeketwa hivyo basi hutaka kudadisi tofauti iliyopo, ambapo, wanaume wa asili ya bara huwadekeza na utofauti huo unapoibuka, basi husimuliana kwa vikao na kuwachochea wenzao.

Nastehe Aftin, mwanaharakati dhidi ya ukeketaji anasema kuwa wanawake wanaoishi katika jamii zinazokeketa wamefedheshwa katika ndoa.

“Katika utafiti tuliofanya, kati ya wanawake kumi katika jamii, nane wako na msongo wa mawazo kutokana na kufedheheshwa katika ndoa, na wanaume wanaoshinikiza ukeketaji ndio wanaochangia haya yote,” anasema.

Bi Aftin anasema kuwa ukeketaji sio suluhisho la kuchepuka kwani mwanamke aliyekeketwa angali ana hisia kama wanawake wengine, tofauti ikiwa katika mtiririko wa zile hisia wakati wa kujamiiana.

Anadai kuwa wanaume katika jamii husika hawachukui muda wao katika mchakato huo, kwani punde tu wanaporidhika, hufuata shughuli zao.

“Wanawake hawa nao wanaogopa kulalamika sababu hapo hapo ataitwa kahaba na apigwe, sasa wanakuja kuyazungumza kwa vikao na pengine wakitafuta kuni msituni ili kupunguza dhiki yao,” anasema.

Hata hivyo, anawarai wanaume waliowaoa wanawake waliokeketwa kuchukua muda wao wakati wa kujamiiana ili kusawazisha hisia za kila mmoja.

Pia, anazirai jamii kuacha ukeketaji akisema dhana yake potovu ni bayana haina msingi wowote.

Sheikh Madobe ambaye pia ni mpinga ukeketaji anasema kuwa, kwa muda mrefu jamii zimesingizia dini ili kuendeleza udhalimu huo badala ya kufunza maadaili halisi.

“Sio dini, sio Sunah, haitunzi ubikra na wala haizuii kuchepuka, tuache ukeketaji na tufunze watoto wetu maadili ya dini kikamilifu,” anasema.

Pia, anawarai wanaume kurejea katika maelekezo ya dini kuhusu jinsi ya kuishi na wake zao, jinsi ya kuwapenda na kuwatunza ili kupuzilia mbali haramu ambayo imeanza kusheheni.

 

  • Tags

You can share this post!

JKT Queens wadhihirisha ndio malkia wa kweli CECAFA baada...

Msiuze mahindi mpaka tuwatangazie bei, Serikali yaambia...

T L