• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 6:50 AM
Jaji Mkuu: Uamuzi wa usiku watatiza Koome

Jaji Mkuu: Uamuzi wa usiku watatiza Koome

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Martha Koome jana alijitetea mbele ya Tume ya Huduma za Mahakamani (JSC), kuhusu uamuzi aliotoa usiku na kuruhusu uchaguzi wa marudio wa urais mnamo 2017.

Uchaguzi huo ulikuwa umesitishwa na mahakama kuu.

Akijibu maswali ya Kaimu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu, jaji huyo alisema alipigiwa simu na aliyekuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa, ambaye sasa ni Mwanasheria Mkuu, Paul Kihara Kariuki kurudi Nairobi.

Alisema alitoka Malindi usiku na akasafiri hadi Nairobi kusikiza kesi hiyo bila idhini ya aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, lakini akajitetea kuwa alikubali kufanya hivyo ili kuokoa nchi.

“Ilibidi niokoe nchi hii isitumbukie katika vita na mtafaruku wa kisheria kwa kuamuru zoezi la uchaguzi liendelee,” alisema Jaji Koome. Kando na hayo, alitakikana pia kujibu kuhusu uamuzi wake wa awali ambao ulisema, sio hatia mwananchi kuungama hadharani kwamba ni shoga.

Akitetea uamuzi huo aliotoa katika kesi ya shirika moja la kutetea haki za mashoga na wasagaji, Jaji Koome alisema kila mmoja yuko huru kuchagua atakachotaka kuwa katika jamii.

Hata hivyo, Jaji Koome alisema hatasita kutoa adhabu kwa wale wanaokaidi kipengee nambari 163 cha sheria za uhalifu kinachoharamisha vitendo vya ushoga na usagaji.

Aliongeza kusema kesi hiyo ingali katika mahakama, hivyo basi hangejadili mengi zaidi kuihusu. Jaji Koome ndiye watatu kuhojiwa na JSC katika mchakato wa kutafuta atakayemridhi Jaji Maraga, ambaye alistaafu rasmi mapema mwaka huu.

You can share this post!

Njama mpya yachorwa kutimua Ruto Mlima Kenya

Wizara yataka Wakenya waliopoteza ajira walipwe na serikali