• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Je, mkataba wa kibiashara baina ya Kenya na Uingereza utawafaa wakulima wadogo?

Je, mkataba wa kibiashara baina ya Kenya na Uingereza utawafaa wakulima wadogo?

Na SAMMY WAWERU

WIKI moja baada ya muungano wa wakulima wadogowadogo nchini (KSSF) kupuliza kipenga kuhusu uhalisia wa mkataba kati ya Kenya na Uingereza kuruhusu biashara ya bidhaa za kilimo, serikali haijatoa mwelekeo wala kauli yake.

Mwaka uliopita, 2020 mataifa haya mawili yalifanya mazungumzo kuafikiana kuendeleza biashara huru ya bidhaa za kilimo na nyinginezo.

Wakulima wa Kenya wanalalamikia kuwekwa gizani kuhusu yaliyojadiliwa.

“Kipindi cha mazungumzo, Uingereza ilihamasisha wananchi wake kuhusu yaliyomo. Kenya hatukuelezwa,” amesema Bw Justus Lavi, Katibu wa Kitaifa, KSSF.

Akilalamikia kukosa ufahamu wa yaliyomo kwenye mkataba huo, Bw Lavi amesema huenda kuruhusiwa kuingia kwa bidhaa za kilimo kutoka Uingereza kutaathiri soko la mazao ya humu nchini.

“Sisi kama wakulima wadogo tutakosa soko la mazao yetu, yale ya Uingereza yakisheheni nchini bila kudhibitiwa,” akaambia Taifa Leo Dijitali, kupitia mahojiano ya kipekee.

Bw Davies Nyachieng’a, afisa katika kitengo cha biashara na uwekezaji, Eco-News Africa. Picha/ SAMMY WAWERU.

Kulingana na Lavi, na ambaye ni mkulima wa mseto wa mimea, wakulima na wadauhusika hasa katika vyama na miungano ya wakulima, hawakushirikishwa katika mazungumzo ya mkabataba huo wa kibiashara.

“Umma haikushirikishwa kutoa maoni. Mamia, maelfu na mamilioni tunaotegemea shughuli za kilimo tutaumia,” akalalama, akiongeza kwamba nafasi za kazi katika sekta ya kilimo nchini zitapungua

Shirika la kijamii la Eco-News Africa, lisilo la kiserikali, limeungana na KSSF kutetea maslahi ya wakulima Kenya.

Uingereza ni nchi iliyoboresha sekta ya kilimo, ambapo hupiga jeki wakulima wake kwa pembejeo kama vile mbegu, fatalaiza na dawa.

Mikakati hiyo haipo nchini, licha ya kuwa sekta ya kilimo na ufugaji imegatuliwa.

“Hii ina maana kuwa mazao na bidhaa za kilimo kutoka Uingereza yakiingia, yatakuwa ya bei ya chini. Wakulima wetu ndio wataumia,” akaonya Davies Nyachieng’a, afisa wa kitengo cha biashara na uwekezaji, Eco-News Africa.

Mkataba huo uliidhinishwa kuwa sheria mapema 2021, ila haujaanza kutekelezwa.

Aidha, Eco-News Africa inatilia shaka pupa za serikali kuupitisha, na hata kuuwasilisha katika bunge la Jamii ya Muungano wa Afrika Mashariki (EAC).

“Nchi wanachama wa EAC zilipaswa kuujadili kwa kina, kabla kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa bunge hilo,” Nyachieng’a akapendekeza.

Kwa upande wa KSSF, Justus Lavi anatahadharisha endapo sheria na mikakati faafu hataiwekwa kudhibiti uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka nje ya nchi, huenda kukawa na mlipuko wa zile bandia.

“Kutakuwa na usindikaji mwingi wa mazao na bidhaa za kula. Ni hatari kwetu sisi wenyewe na nchi jirani,” akaonya.

“Wafanyabiashara wahuni watatumia mwanya huo kuibuka na bidhaa ghushi. Ndio maana visa vya Saratani nchini vinazidi kuongezeka,” Lavi akaelezea.

Uagizaji wa kuku na mayai kutoka nje ya nchi, bila mipangilio faafu umetajwa kuchangia kuathirika kwa ufugaji wa kuku Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Bawabu aliyeingia kwa nyumba aliyolinda kusaka chakula...

‘Corona imenisukuma kwa kona’