• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Kaburi la Mekatilili sasa kugeuzwa ‘chuo’ cha utamaduni

Kaburi la Mekatilili sasa kugeuzwa ‘chuo’ cha utamaduni

Na MAUREEN ONGALA

WAZEE wa Kaya wameanzisha mikakati ya kuhifadhi kaburi la shujaa wa jamii ya Mijikenda, Mekatilili wa Menza, lililo Bungale katika eneobunge la Magarini.

Wazee hao wanalenga kufanya kaburi hilo kama kivutio cha watalii.

Pia sehemu hiyo itakuwa eneo la kutoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusu mila na tamaduni za jamii ya Wagiriama.

Mekatilili wa Menza alijulikana kwa ushujaa wake wa kuongoza jamii ya Wagiriama kupigania uhuru wakati wa ukoloni.

Alizikwa mwaka 1924 baada ya kuongoza jamii hiyo katika vita maarufu ‘Giriama Uprising’ kati ya mwaka wa 1913-1914.

Kaburi lake lipo katika sehemu inayofahamika kama Ulaya Kwa Jele.

Mekatilili wa Menza alitoka katika jamii ya Amwamkare.

Kwa miaka mingi kaburi hilo lilitumiwa kwa ukumbusho wa shujaa huyo na jamii ya Wagiriama lakini kwa muda sasa lilikuwa limeachwa bila kushugulikiwa.

Kila mwaka jamii hiyo husherehekea siku kuu ya makumbusho ya Mekatilili wa Menza.

Sehemu hiyo ina lango linalokuelekeza katika jengo la pekee Ulaya Kwa Jele kijini Bungale, eneobunge la Magarini.

Jengo hilo la saruji lilijengwa na shirika la kuhifadhi mazingira lisilo la serikali la Nature Kenya.

Nyumba za kitamaduni zilizokuwa katika maeneo hayo zimeanguka huku kaburi la shujaa huyo likiwa limeharibika na kujaa nyasi na magugu.

Wakiongozwa na mshirikishi wa muungano wa wazee wa Kaya, Bw Tsuma Nzai, wazee hao pamoja na familia ya shujaa huyo walifanya matambiko maalum kutakasa kaburi hilo.

Kulingana na Bw Nzai, jamii ya Mekatilili walisema ni wakati mwafaka wa kutunza kaburi hilo kwani lina historia maalum kwa jamii ya Wagiriama na Wakenya kwa jumla.

“Familia wameamua kuwa yetote atakayetaka kumsherehekea mama yao ni lazima aandae sherehe katika maeneo ya makaburi yake,” akasema Bw Nzai.

Alitoa wito kwa viongozi katika jamii kujitokeza na kuboresha maeneo kama hayo kwa manufaa ya kizazi kijacho na cha sasa.

Alisema kufanya matambiko maalum na maombi katika kaburi hilo huaminika kutoa visirani na majanga ambayo yanaandama jamii hiyo.

Baadhi ya wazee wa Kaya husherekea shujaa huyo katika eneo la Shakahola eneobunge la Magarini ambapo alimpiga mzungu kofi.

Kitukuu wa Mekatilili wa Menza, Bw Alphonse Jefwa, alikosoa serikali ya taifa kwa kukosa kutambua familia ya shujaa huyo.

“Shujaa Mekatilili alikuwa mwanamke ambaye alihusika katika kupigania uhuru nchini. Alipoaga dunia aliacha familia ambayo kwa sasa ni kubwa, lakini serikali haijatutambua,” akasema.

Kulingana na Mzee Jinathan Wanje, jamii ilimsherehekea sana Mekatilili enzi ya aliyekuwa waziri, marehemu Karisa Maitha.

Baada ya kifo cha Maitha, sherehe hizo zilisitishwa ghafla bila wazee hao kufahamishwa.

“Tunataka kurekebisha kaburi la Mekatilili kwa sababu kuna hatari ya kuwa litasahaulika na hata kupotea kwa sababu halijahifadhiwa,” akasema.

Familia ya Mekatilili wa Menza ina mipango ya kuanzisha wakfu ili kuwasaidia watoto kutoka familia maskini kuendeleza masomo yao, na kutunza maswala ya jamii ya Wagiriama.

You can share this post!

Bayern Munich waduwazwa na Augsburg ligini

Mwatate FC yajipanga kupanda ngazi ligi kuu ya FKF licha ya...

T L