• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Kafyu yasaidia kuepusha hali mbaya shughuli ya utoaji chanjo ikiendelea – Kagwe

Kafyu yasaidia kuepusha hali mbaya shughuli ya utoaji chanjo ikiendelea – Kagwe

Na SAMMY WAWERU

AMRI ya kitaifa ya kutotoka nje kati ya saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri itaendelea kutekelezwa kwa muda wa siku 30 zaidi.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza Jumatatu, kuongezwa kwa muda huo wa kafyu kutaiwezesha serikali kutoa chanjo zaidi.

Tangazo hilo limejiri licha ya baadhi ya viongozi na wanasiasa, wadau katika sekta mbalimbali kuitaka serikali kufungua uchumi kikamilifu.

“Tumeongeza muda wa utekelezaji kafyu na sheria zinginezo kuzuia msambao wa virusi vya corona kwa siku 30 zaidi, ili tuweze kutoa chanjo kwa watu wengi iwezekanavyo,” akasema Bw Kagwe.

Alisema hayo jijini Nairobi, wakati akizindua rasmi sheria ya afya ya umma na jamii itakayotolewa na Shirika la Kuimarisha Huduma za Jiji la Nairobi (NMS).

Akitetea kuendelea kutekelezwa kwa kafyu ya kitaifa na mikakati ya kuzuia kuenea kwa Covid-19, waziri Kagwe alisema hatua hiyo pia inasaidia kulinda maisha ya Wakenya.

Kanuni hizo zilianza kutekelezwa mwaka 2020 mara baada ya Kenya kuthibitisha kisa cha Covid-19.

“Jukumu la kulinda Wakenya si la Mutahi Kagwe wala Rais Uhuru Kenyatta pekee, ni letu sisi sote,” waziri akasema.

“Watu wafahamu kuwa wamekodolewa macho na ugonjwa hatari,” akatahadharisha.

Kauli ya Bw Kagwe imejiri kipindi ambacho viongozi na wanasiasa wakiongozwa na Rais Kenyatta, Naibu wa Rais Dkt William Ruto, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kati ya wengineo wanaendelea kuandaa mikutano ya umma, katika kile kinachonekana kama mchakato wa kampeni za 2022.

You can share this post!

Mshindi wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Hegerberg,...

Leeds United wakung’uta Watford na kusajili ushindi...