• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Leeds United wakung’uta Watford na kusajili ushindi wao wa kwanza ligini msimu huu

Leeds United wakung’uta Watford na kusajili ushindi wao wa kwanza ligini msimu huu

Na MASHIRIKA

LEEDS United walisajili ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwacharaza Watford 1-0 mnamo Jumamosi uwanjani Elland Road.

Bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo lilipachikwa wavuni na beki Diego Llorente aliyekuwa akirejea ulingoni baada ya kupona jeraha. Llorente aliyejeruhiwa paja wakati wa mechi ya awali dhidi ya Liverpool, alichuma nafuu kutokana na masihara ya mabeki wa Watford na kujaza kimiani mpira uliombabatiza Juraj Kucka.

Ingawa Watford walifunga bao katika kipindi cha pili, goli hilo halikuhesabiwa na refa kwa madai kwamba lilifumwa wavuni wakati ambapo kipa Illan Meslier alikuwa amechezewa vibaya.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Leeds United kuondoka uwanjani Elland Road wakijivunia alama tatu kwenye kampeni za muhula huu. Stuart Dallas alipata nafasi nyingi za kufunga mabao ila juhudi zake zikazimwa na kipa wa Watford, Ben Foster ambaye pia aliwajibishwa mara kadhaa na fowadi wa zamani wa Manchester United, Daniel James.

Leeds United kwa sasa wanashikilia nafasi ya 16 jedwalini kwa alama sita sawa na Crystal Palace. Watford kwa upande wao wanakamata nafasi ya 14 kwa alama saba sawa na Leicester City ya kocha Brendan Rodgers.

  • Tags

You can share this post!

Kafyu yasaidia kuepusha hali mbaya shughuli ya utoaji...

ODONGO: Kanu ina kibarua kurejelea umaarufu wake wa awali