• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kanisa lajitenga na mwanamume anayedaiwa kuwachoma wavulana 3

Kanisa lajitenga na mwanamume anayedaiwa kuwachoma wavulana 3

NA FLORAH KOECH

KANISA la Deliverance limekanusha kuwa mwanamume aliyedaiwa kuwachoma wavulana watatu wa shule kwa kushukiwa kuiba keki za Sh80, alikuwa ni mmoja wa wachungaji wake.

Tukio hilo liliripotiwa katika kijiji cha Kaptimbor, viungani kwa mji wa Kabarnet, Kaunti ya Baringo wiki iliyopita.

Msimamizi wa kanisa hilo eneo la Kerio, Padre John Sawe, alisema kwamba mshukiwa kwa jina Joseph Mduma, hakuwa pasta bali mshirika, kabla ya kuhama kanisa hilo.

Hata hivyo, Bw Sawe alithibitisha kisa hicho akisema kuwa adhabu iliyopatiwa wavulana hao ilikuwa ya kinyama na kinyume cha mafunzo ya kanisa hilo.

“Tumehuzunishwa na ripoti kwamba baadhi ya wavulana walichomwa kwa madai ya wizi na tunalaani vikali kisa hicho,” alisema.

Mshukiwa

“Mshukiwa, anayetajwa kuwa pasta sio mmoja wetu kamwe. Alikuwa mshiriki katika kanisa letu zamani kabla ya kuhama. Viongozi wote wa makanisa yetu wako na vitambulisho na wanajulikana na umma,” alisema Padri Sawe.

Alisema kwamba kanisa la Deliverance lina utaratibu wake na mapasta wake wana maadili.

“Aliyekuwa akionyeshwa katika vyombo vya habari si pasta wa kanisa letu la Kabarnet na hatuko na tawi lingine katika mji huo,” alisema.

Pasta Henry Kipng’ok wa kanisa la Deliverance mjini Kabarnet, alisema kwamba wana utaratibu wa kutawaza mapasta, na akaongeza kuwa Bw Mduma alikuwa tu mcheza piano katika kanisa hilo kabla ya kuhama.

Utaratibu wa kanisa

“Huwa tunatawaza mapasta wetu na mwanamume anayedaiwa kuwa pasta katika kanisa hili alikuwa tu mcheza piano miaka iliyopita na akatoweka. Tunataka kuambia ulimwengu kwamba si pasta wa kanisa letu inavyodaiwa. Vyombo vya habari vinafaa kukoma kupaka tope kanisa la Deliverance kwa kuwa tuko na jina ambalo tumejenga kwa miaka mingi,” akasema Bw Kipng’ok.

Mshukiwa huyo pamoja na mwenzake Daniel Cherop, ambaye ni mwajiriwa wake, wanalaumiwa kwa kuchoma wavulana watatu kwa madai waliiba pakiti ya keki ya Sh80 kutoka duka lake Jumanne usiku.

Inadaiwa kuwa wawili hao pamoja na mshukiwa mwingine ambaye anasakwa, waliwachoma watoto hao miguu.

Wavulana hao wanatibiwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Baringo wakiwa na majeraha mabaya ya moto.

  • Tags

You can share this post!

Wapinzani watoa habari za uongo kunivuruga – Kidero

Kindiki ahimizwa akubali uwaziri Ruto akishinda urais Agosti

T L