• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Kibaki alipofika kortini kujitetea

Kibaki alipofika kortini kujitetea

JOSEPH WANGUI Na MERCY MWENDE

IJAPOKUWA watu wengi walimwona Rais Mstaafu Mwai Kibaki kama tajiri mkubwa, aliwashangaza wengi alipofika mahakamani kutetea mgao wake katika kampuni ndogo waliyoanzisha na marafiki wake saba.

Mzozo huo ulimfanya Rais Kibaki kufika katika mahakama moja mjini Nyeri, ambako kesi hiyo ilikuwa ikiendelea.

Bw Kibaki alifika katika Mahama ya Mazingira na Ardhi mnamo Septemba 2013, miezi sita baada ya kustaafu kama rais.

Kwenye kikao cha mahakama, alitoa ushahidi kuhusu uongozi na utaratibu wa umiliki katika kampuni ya Mathingira Wholesalers Ltd, waliyoanzisha na marafiki wake mnamo 1976.

Kampuni hiyo ilibuniwa miaka miwili baada ya Mzee Kibaki kuhamisha ngome na shughuli zake za kisiasa kutoka Nairobi hadi nyumbani kwake, eneo la Othaya, Nyeri.

Kwenye ushahidi wake mbele ya Jaji Anthony Ombwayo, Bw Kibaki alilenga kulinda mgao wake katika kampuni hiyo na jengo la orofa moja lililo mjini Nyeri, karibu na afisi ya chama cha Kanu.

Jengo hilo lina biashara kadhaa kama maduka, hoteli, baa na vichinjio, ambapo huzalisha pato la Sh200,000 kwa mwezi.

Bw Kibaki aliibuka kuwa rais wa kwanza aliyestaafu nchini kufika mahakamani kulinda biashara yake.

“Rais Mstaafu analinda na kutetea haki yake ya kifedha. Uamuzi kwenye kesi hiyo utatolewa kulingana na ushahidi atakaotoa, ikizingatiwa yeye ni mmoja wa wamiliki wa mali hiyo,” akasema wakili Gibson Kamau Kuria, aliyemwakilisha Bw Kibaki katika kesi hiyo.

Kufikia kifo chake Ijumaa, yeye pamoja na waanzilishi wengine wa jengo hilo bado hawakuwa wameanza kufaidika kutokana na kodi zinazolipwa tangu 2014.

Hii ni baada ya mahakama kuagiza kodi hiyo iwe ikielekezwa kwa akaunti ya pamoja yenye majina ya mawakili wanaowawakilisha walalamishi kabla ya kutoa uamuzi wake.

Majuzi, Dkt Kuria aliwasilisha ombi mahakamani, akiitaka kumruhusu kupata fedha hizo ili kuwagawia wamiliki.

Hata hivyo, mahakama bado haijatoa uamuzi wake kuhusu ombi hilo.

Dkt Kuria aliwasilisha ombi hilo kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, ambao ulirejesha umiliki wa mali hizo kwa Bw Kibaki na marafiki wake.

Wakili huyo alisema mahakama iliwazuia na Bw Kibaki na kuingilia shughuli za kampuni hiyo kwa vyovyote vile kwa miaka 14.

Marafiki hao ni Bw Kimwatu Kanyungu, Francis Gathungwa, Gadson Gitonga Mbuthia, Kiiru Gachuiga, Kibera Gatu, Philip Gichuhi na Muriithi Nganga.

  • Tags

You can share this post!

Mzee Kibaki aunganisha Azimio, UDA

Mzazi aliyepinga CBC kortini ajiondoa, waziri Magoha sasa...

T L