• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Kijana anayelenga kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo

Kijana anayelenga kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo

Na JOHN KIMWERE 
NI kati ya wasanii wengi tu wa kiume wanaojituma mithili ya mchwa katika tasnia ya uigizaji wakipania kuibuka wanamaigizo mahiri miaka ijayo.
Sina budi kutaja kuwa taifa hili limefurika vijana wengi tu wenye vipaji vya kuigiza walivyotunukiwa na Karima lakini baadhi yao bado hawajafanikiwa kukubalika wala kutambuliwa.
Robert Obonyo Chybre anaorodheshwa miongoni mwa waigizaji wanaodhamiria kusaidia wenzao kupata mwelekeo katika sekta ya maigizo.
 
MSANII NA MWALIMU
Amehitimu kwa shahada ya digrii katika masuala ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) ambapo amekuwa mwalimu kwenye Shule kadha wa kadha za Upili ikiwamo Shule ya Sunshine, Lang’ata, Nairobi.
Pia ni edita wa filamu na produsa anayelenga makubwa. Kando na hayo anamiliki chaneli ya Youtube iitwayo Nairobi Chronicles aliyoanzisha mwaka 2018 ambapo huitumia kupeperusha filamu fupi.
Msanii Robert Obonyo Chybre…Picha/JOHN KIMWERE
 Alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Lakini alipata kunoa kucha zake katika usanii alipojiunga na Kundi la Talent House Production chuoni humo mwaka 2015.
”Ninaamini ninatosha mboga katika masuala ya uigizaji ambapo ninalenga kuibuka kati ya wana maigizo nguli hapa nchini na Afrika kwa jumla. Uigizaji ni burudani pia ajira kwa wengi wetu wenye talanta,” alisema na kuongeza analenga kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.
 SITAKI INGINE, NIMECHOKA
Anadokeza kuwa mwigizaji Raymond Ofula wa humu nchini ndiye aliyechangia avutiwe na maigizo. Kutokana na kushikika katika taaluma ya ualimu msanii huyu anasema kuwa hakupata nafasi ya kufanya kazi na makundi mengi ila aliwahi shiriki filamu fupi katika kipindi cha House helps of Kawangware.
Kipindi hicho awali kilikuwa kinapeperushwa kupitia KTN kisha NTV ya Nation Media Group (NMG). Obonyo ambaye tangia utotoni mwake alidhamiria kuwa msanifu kupitia chaneli yake amepeperusha filamu fupi nyingi tu ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka mitano.
Baadhi yazo zikiwa: ‘Tabia za watu kuomba pesa in CBD,’ ‘Sponsor and Campus girl,’ ‘Sitaki, siko kwa moods,’ ‘Mkipata mnashare slayqueen nyinyi wote,’ na ‘Sitaki ingine, nimechoka,’ kati ya zingine.
Pia amefanikiwa kushiriki vipindi kadhaa ambazo zimepeperushwa kupitia runinga tofauti ikiwamo ‘Wacha Ufala’ na ‘Yes Mwalimu’ (KU TV) pia  (Ibru TV).
 
 DENZEL WASHINGTON
Analenga kumiliki studio ya kuzalisha filamu za nguvu pia aibuke kati ya maprodusa mahiri nchini. Anasema anatamani sana kutinga kiwango chake Denzel Hayes Washington mzawa wa Marekani aliyepata umaarufu kutokana na filamu mbali mbali ikiwamo ‘Equalizer.’
Kama kawaida anasema changamoto ni tele maana wapo wasanii wengi tu wanaozidi kuhangaika kwa kukosa ajira. ”Kwa ndani ya kipindi hiki cha janga la corona kupata ajira ya uigizaji sio rahisi.
Pia ningependa kutoa wito kwa vyombo vya habari hasa mashirika yanayomiliki runinga kuanzisha vipindi nyingi vya kupeperusha filamu za wazalendo ili kutoa nafasi za ajira kwa wasanii wanaoibukia,” akasema.
  • Tags

You can share this post!

Ulinzi starlets: Tuna uwezo kutwaa ligi kuu

Shinikizo DPP Noordin Haji ang’atuke yapelekewa PSC

T L