• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Lalama utatuzi masuala ya Tsavo unakawia

Lalama utatuzi masuala ya Tsavo unakawia

NA LUCY MKANYIKA

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta, imelalamikia jinsi utatuzi wa masuala tata kati yake na serikali ya kitaifa kuhusu Mbuga ya Tsavo unaenda mwendo wa kobe.

Naibu Gavana, Bi Christine Kilalo, alisisitiza haja ya baadhi ya masuala yanayojadiliwa katika Kamati ya Kiufundi ya Mahusiano ya Kiserikali (IGRTC) kushughulikiwa na ngazi za juu serikalini ili kutatuliwa upesi.

Baadhi ya masuala ambayo kaunti hiyo imekuwa ikilalamikia ni kama vile ugavi wa mapato yanayopatikana Tsavo, na fidia kwa waathiriwa wa uvamizi wa wanyamapori.

Wito huu Bi Kilalo umetokea siku chache kufuatia agizo la Rais William Ruto, kwa wizara ya utalii na serikali ya kaunti kushiriki mazungumzo, lengo likiwa ni kaunti kupokea asilimia 50 ya mapato ya mbuga hiyo.

“Kuna nia njema ya kutatua masuala haya lakini kuna baadhi ya wadau ambao hawajashirikishwa kwa mchakato huu wa kutafuta suluhu, kwa hivyo itakuwa vigumu kutatua masuala hayo,” akasema Bi Kilalo.

Naibu Gavana alielezea wasiwasi wake kuhusu mchakato wa upatanisho wa muda mrefu na kusisitiza haja ya kuharakisha mazungumzo.

“Tunataka kuona mwisho wa mchakato huu kwa hivyo ikiwa kuna mambo ambayo hatuwezi kukubaliana basi tuyapeleke kiwango cha juu,” alisema.

Kwa upande wake, IGRTC ilisisitiza dhamira yake ya kusuluhisha mzozo huo.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw John Kimwela, alisema watashauriana na kuandaa Mkataba wa Makubaliano kwa masuala yaliyokubaliwa kufikia sasa ili yaanze kutekelezwa.

“Tutafanya chochote itakachogharimu kuhakikisha kuwa suala hili linafungwa na tutazingatia manufaa ya wenyeji wa Kaunti ya Taita Taveta na taifa kwa jumla,” akasema.

Katika mjadala huo, masuala mengine yaliibuliwa, ikiwa ni pamoja na fidia kutolewa kwa wakati bora, mgogoro wa mipaka na ardhi na KWS, uchimbaji madini katika mbuga hiyo, nafasi za kazi kwa wenyeji, uzio wa mbuga kujengwa ili kuzuia wanyamapori kuvamia maeneo ya makazi, wajibu wa Mashirika kwa Jamii (CSR), na masuala mengine muhimu yanayohusiana na hayo.

 

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Haifai kuweka shule za chekechea pamoja na...

Asante Mlima Kenya kwa kukataa kuwa mateka wa Uhuru...

T L