• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Leicester City wakomoa Brentford na kupaa hadi 10-bora katika jedwali la EPL

Leicester City wakomoa Brentford na kupaa hadi 10-bora katika jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

TIMOTHY Castagne na James Maddison walifunga bao kila mmoja na kusaidia waajiri wao Leicester City kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Brentford katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili.

Ushindi huo ulipaisha Leicester wanaotiwa makali na kocha Brendan Rodgers hadi nafasi ya 10 jedwalini kwa alama 10 sawa na Aston Villa.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Castagne ambaye ni raia wa Ubelgiji kuchezea Leicester mwaka huu wa 2022 tangu apate jeraha la mguu mwishoni mwa 2021. Bao lake dhidi ya Brentford lilitokana na krosi aliyoandaliwa na Harvey Barnes katika dakika ya 20.

Maddison alifunga bao la pili la waajiri wake kupitia mpira wa ikabu katika dakika ya 33. Leicester walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakitinga robo-fainali za Europa Conference League mnamo Machi 17, 2022 baada ya kudengua Rennes ya Ufaransa.

Brentford walifutiwa machozi na Yoane Wissa mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kushirikiana vilivyo na Bryan Mbeumo.

Bao hilo liliwapa Brentford motisha zaidi ya kuvamia wageni wao ila kipa Kasper Schmeichel akasalia imara na kupangua makombora kadhaa aliyoelekezewa na Tariqe Fosu.

Leicester wamesuasua pakubwa katika kampeni za msimu huu tangu uthabiti wa safu yao ya ulinzi ulemazwe na wingi wa visa vya majeraha. Beki Wesley Fofana aliwajibishwa na Leicester kwa mara ya kwanza msimu huu katika gozi la Europa Conference League dhidi ya Rennes mnamo Machi 17.

Castagne naye alikuwa mkekani tangu Disemba 28, 2021 na aliondolewa uwanjani katika kipindi cha pili dhidi ya Brentford na nafasi yake kutwaliwa na Jonny Evans ambaye pia alikuwa akitandaza mchuano wake wa kwanza tangu Disemba 12, 2021.

Kiungo Wilfred Ndidi sasa anatarajiwa kukosa mechi zote zilizosalia msimu huu baada ya kupata jeraha baya la goti dhidi ya Rennes.

Ingawa Leicester wana matumaini finyu ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa saba-bora na kufuzu kwa soka ya bara Ulaya muhula ujao, wapo pazuri kutia kapuni ubingwa wa kipute kipya cha Europa Conference League. Watavaana na PSV ya Uholanzi katika hatua ijayo ya nane-bora.

Maddison sasa anashikilia rekodi ya kufunga jumla ya mabao 13 ya EPL kwa kuvurumisha makombora mazito nje ya kijisanduku tangu aingie katika sajili rasmi ya Leicester mnamo 2018-19.

Brentford waliokosa huduma za kiungo Christian Eriksen anayeugua Covid-19, walishuka ugani wakiwa na lengo la kushinda mechi tatu mfululizo katika EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 75. Sasa wanakamata nafasi ya 15 kwa alama 30 na wako katika hatari ya kupitwa na Leeds United pamoja na Everton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Hatukudhamini utafiti wa Infotrak kwa nia mbaya, Haki...

Bajeti kusomwa Aprili 7

T L