• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 10:36 AM
Mackenzie kuendelea kufungiwa ndani serikali ikisema uchunguzi haujakamilika

Mackenzie kuendelea kufungiwa ndani serikali ikisema uchunguzi haujakamilika

NA BRIAN OCHARO

MHUBIRI anayehusishwa na vifo vya vya Shakahola, Paul Mackenzie, na washukiwa wenzake 29 wataendelea kuzuiliwa na polisi huku serikali ikitaka afungiwe kwa siku 180 zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

Haya yanajiri wakati ambapo imeibuka kwamba mchakato wa kisayansi wa kutambua miili 429 iliyofukuliwa msituni Shakahola huenda uchukue angalau miezi sita kukamilika. Serikali inasema matokeo ya uchunguzi wa chembechembe za DNA ndio yatabaini mashtaka halisi ya kumfungulia mhubiri huyo na wenzake “ili kutoa fursa ya haki kutendeka kwa waathiriwa.”

Washukiwa hao wamekuwa rumande tangu Aprili mwaka huu walipokamatwa kutokana na vifo vya mamia ya watu wanaodaiwa walikuwa waumini wa Kanisa la Good Life International linalohusishwa na Bw Mackenzie.

Mahakama sasa inasubiriwa kutoa uamuzi kuhusu kuendelea kuzuiliwa kwa washukiwa hao.

Manusura 65 ambao wengine wao sasa wamekuwa washukiwa wa mauaji ya Shakahola pia wamekuwa rumande kwa karibu miezi miwili sasa baada ya kuondolewa katika Kituo cha uokoaji cha Sajahanad huko Mtwapa.

Serikali imeeleza kuwa, baadhi ya manusura hao watashtakiwa kwa makosa ya jinai baada ya kushindwa kueleza waliko watoto wao na jamaa zao ambao waliondoka nao kwenda msituni lakini hawajawahi kupatikana.

Serikali imedai kuwa, washukiwa hao walitenda makosa ya mauaji, kujaribu kuua, kuua bila kukusudia, kusaidia kujiua, kusababisha madhara makubwa kwa watoto, itikadi kali, ukatili na kutelekeza watoto.

Upande wa mashtaka pia umesema kuwa watu hao watashtakiwa kwa makosa mengine ikiwemo kushindwa kuwapa watoto mahitaji yao, kushindwa kuwapeleka shuleni, kutotoa taarifa za kifo na kuzika watu bila kibali.

Kizuizi hicho cha muda mrefu pia kilitolewa ili kuruhusu polisi kukamilisha uchunguzi ambao ulijumuisha uchambuzi na ulinganishaji wa sampuli za DNA za watuhumiwa na marehemu ili kujua uhusiano wa kinasaba na wa kifamilia.

Miezi miwili iliyopita, Mackenzie na washirika wake waliandamana mahakamani kupinga kuwekwa rumande muda mrefu bila kushtakiwa.

Walitatiza shughuli za mahakama wakiimba kauli mbiu “Haki Yetu” mara tu walipogundua kuwa serikali ilikuwa na nia ya kufanya maombi ya kuwazuilia kwa siku 47 zaidi.

Kwa zaidi ya dakika tano, Mackenzie na wafuasi wake walifanya maandamano makubwa huku wakidai haki zao.

Serikali, hata hivyo, imeunga mkono hatua ya kuwazuilia watu hao ikisema itasaidia kulinda usalama wa taifa kwani kuna uwezekano kwamba ikiwa wataachiliwa huru, wanaweza kuendelea kuwafunza watu wengine itikadi kali.

Mahakama pia imekubaliana na serikali kwamba matukio yanayoendelea kule Shakahola yamepata sifa mbaya na kusababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi kwa ujumla.

Mahakama ilikuwa imeambiwa kwamba watu hao walitoa taarifa za uongo kwa wapelelezi ikiwa ni pamoja na majina ya uongo ya jamaa zao.

Watoto wote waliopotea wana umri kati ya mwaka mmoja na 14. Serikali imeiambia mahakama kuwa watoto walionusurika kwenye mfungo huo mbaya wamesaidia wapelelezi kukusanya ushahidi wa kutosha dhidi ya washukiwa hao wote.

  • Tags

You can share this post!

Ghasia zazuka katika hafla ya kanisa la Gavana

Kenya yapokea vifaa vya kidijitali kuimarisha uangalizi wa...

T L