• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
Madereva watundu wanaoibia wachuuzi

Madereva watundu wanaoibia wachuuzi

NA RICHARD MAOSI

WAFANYABIASHARA wa mapato ya chini eneo la Gitaru, barabara ya Nairobi-Nakuru wameripoti visa vya baadhi ya madereva kutoroka bila kulipia bidhaa zao.

Changamoto hiyo inaathiri sana wachuuzi wanaozimbua riziki kwa kuuzia madereva wanaopita.

Malalamiko ya wachuuzi wa barabara ya Nairobi-Nakuru si tofauti na ya kuelekea Eldoret kutoka Nakuru, ambapo wauzaji mahindi choma na majani chai wanateta kuhusu madereva watundu kuponyoka na jasho lao.

Licha ya hatari kubwa inayowakodolea macho barabarani, wafanyibiashara hao wamekiri kuhangaishwa na madereva wanaojifanya ni wanunuzi.

Bi Ann Warutere muuzaji wa maji Gitaru anasema kwa sababu ya hali ngumu ya maisha, wachuuzi wengi wamekuwa wakitumia mbinu ya kuwashawishi wanunuzi hadi kwenye barabara kuu.

Isitoshe, hawana sehemu maalum kuuzia bidhaa zao.

Changamoto kubwa hutokea pale wanapokumbana na madereva wezi, wengi wao wakiwa ni wale wanaomiliki magari ya kibinafsi.

“Siku hizi inabidi madereva walipe kwanza kabla ya kumkabidhi kitu la sivyo tunaingia hasara ya kujitakia,” asema Warutere.

Wakati huohuo Ann Chebet ambaye ni muuzaji wa majani chai eneo la Sachangwan barrier kuelekea Eldoret, anaomba madereva kuwa na utu.

Anasema wanaowaibia ni waoga, na huwalenga akina mama na zaidi ya mara moja amepoteza mtaji wake wote.

Kulingana na Chebet, maeneo sugu ni Total, Sachangwan, Kibunja na wakati mwingine katika kituo cha kibiashara cha Londiani barabara ya Nakuru kuelekea Kericho.

Anasema wachuuzi huwa wamechukua bidhaa zenyewe kwa mkopo wakilenga kuzilipia mwisho wa siku baada ya kuuza.

Kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi, vijana wengi hawana mtaji wa kujianzishia biashara zao wenyewe.

“Hakika inauma sana kwa sababu matajiri hudhani kuwa tumekula njama ya kuwaibia,” Chebet anasikitika.

Eneo la Londiani Juni 2023, lilipoteza wachuuzi 50 baada ya kugongwa na trela ambalo lilipoteza mwelekeo.

Mkasa huo unaashiria kwamba wanastahili kujengewa sehemu maalum ya kuuzia bidhaa zao ili kuepuka ajali au kuibiwa bidhaa.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Siasa za atakayemrithi Ruto Bonde la Ufa zashika kasi    

Ambia Samidoh akujengee boma lako, Karen Nyamu aambiwa

T L