• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Mgeni aliye na mashtaka saba ya kunajisi watoto amjibu jaji akitabasamu bila kuonyesha majuto

Mgeni aliye na mashtaka saba ya kunajisi watoto amjibu jaji akitabasamu bila kuonyesha majuto

NA STANLEY NGOTHO

RAIA wa Amerika mwenye umri wa miaka 68 ameshtakiwa kwa kuhusika kwenye msururu wa visa vya kudhulumu watoto kingono miezi 18 baada ya kuachiliwa katika hali ya kutatanisha akitumikia kifungo cha miaka 50 jela.

Mshukiwa, Terry Ray Krieger, almaarufu Guka Terry, ambaye amekuwa akizuiliwa na polisi tangu Novemba 10, 2023 alipokumbwa na shtaka la kudhulumu mtoto kingono katika mahakama ya Mavoko, jana alifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa polisi akiwa katika kiti cha magurudumu.

Mshukiwa alinyimwa dhamana baada ya kukanusha mashtaka saba ya kudhulumu watoto kingono mbele ya mahakimu wawili wa mahakama hiyo.

Polisi walilazimika kumsaidia kushuka gari aina ya Land Cruiser kabla ya kumpeleka kwenye seli moja mahakamani. Mshukiwa huyo alikuwa akiishi katika mtaa wa kifahari wa Great Wall, Mavoko na “marafiki” baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.

Alishtakiwa kwa kumnyanyasa kingono msichana wa miaka mitatu katika mtaa huo kati ya Novemba 6, na 8, 2023. Pia, alishtakiwa kwa kukataa alama zake za vidole kuchukuliwa katika kituo cha polisi cha Athi River kinyume na kifungu cha 55(5) cha sheria ya huduma ya polisi ya Kenya ya 2011.

Akiketi kizimbani kwenye kiti chake cha magurudumu, akivalia shati la rangi ya zambarau, fulana ya kijivu, suruali ya kijivu, viatu vya michezo vyeusi na soksi nyeupe, mshukiwa alitulia akisomewa mashtaka.Wakili wake wa kike alijiondoa katika kesi hiyo dakika za mwisho kutokana na “uzito” wa kesi hiyo.

Bw Krieger alimweleza hakimu kuwa hajui kwa nini wakili wake hakuwa mahakamani.

“Mheshimiwa, sijui kwanini wakili wangu hayupo,” alisema akitabasamu na bila masikitiko.

Hata hivyo, Hakimu Mkuu Mwandamizi Barbra Ojoo alimnyima dhamana akimtaja kuwa mtu hatari na “mtoro” aliye nchini kinyume cha sheria.

“Mshtakiwa ana rekodi ya uhalifu huko Amerika. Adhabu ya mashtaka ya sasa ni kifungo cha jela kisichopungua miaka mitano. Hakuna kilichowasilishwa mbele yangu kuonyesha kwamba, mshukiwa anahitaji matibabu maalum. Ninakataa kumpa dhamana kwa sasa. Kesi itatajwa Novemba 27 2023 kwa maandalizi ya kusikilizwa kikamilifu,” aliamuru hakimu.

Mshukiwa ambaye alifokea wanahabari waliokuwa wakimpiga picha akiwatusi bila kujali makosa yaliyomkabili, pia alikabiliwa na mashtaka mengine sita mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mavoko Bi Mary Gitau yakiwemo ya dhuluma za kingono, kuwa nchini kinyume cha sheria, kushirikisha watoto katika ponografia, kuwatumia watoto kunufaika na ukahaba, na kutangaza uhalifu wa kingono unaoshirikisha watoto kinyume cha sheria ya watoto.

“Mheshimiwa, ninajua kuna mtu aliyeapa kutoa pesa zote zinazohitajika ili nifungwe jela. Haya ni mashtaka ya uongo,” aliambia mahakama.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba, ulikata rufaa kupinga kuachiliwa kwake katika kesi aliyofungwa jela miaka 50 baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kudhulumu watoto kingono.

“Upande wa mashtaka umekata rufaa kupinga kuachiliwa kwake alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka 50 katika gereza kuu la Kamiti,” kiongozi wa mashtaka alisema.

Mshukiwa anazuiliwa katika gereza la Kitengela.

Katika kesi iliyofanya afungwe jela miaka 50 alipatikana na hatia ya kudhulumu kingono mvulana mwenye umri wa miaka 3 na msichana wa umri wa miaka 6 ambao polisi walisema walikuwa majirani wake eneo la Olepolos, kaunti ya Kajiado.

  • Tags

You can share this post!

Mishi Mboko aongoza kurusha ndoano mtandaoni kusajili...

Nyamira sasa yajisimamia kusambaza huduma za maji

T L