• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ajabu ya hedhi za wanawake kuwa na njama ya kuchocheana

Ajabu ya hedhi za wanawake kuwa na njama ya kuchocheana

Na WANGU KANURI

JE, siku zako za hedhi zimewahi kuchochewa na hedhi ya mwanamke mwingine? Wanawake wengi hujipata kwenye hali hii wasielewe kwa nini hedhi zao zitashirikiana (menstrual synchrony) na za wanawake walio na ukaribu nao.

Taifa Leo ilizungumza na wanawake wawili ambao walieleza jinsi hedhi zao huathiriana na za wanawake wengine.

Joy Bilha, 26, anasema, “Kila wakati siku zangu za hedhi zikikaribia na nishirikiane au niwe karibu kwa siku mbili au tatu na mwanamke ambaye hedhi zake zimeanza, zangu pia huanza mapema kuliko nilivyotarajia.”

Iwapo ni marafiki, wanawake tunaosoma nao, au tunaoishi karibu nao, hedhi zangu huanza tukiwa pamoja mara nyingi na mmoja wao.

“Sipendi hali hii hata kidogo kwa sababu hunipata kama sijajitayarisha. Kwa mfano iwapo natarajia hedhi yangu mwishoni mwa mwezi, unapata zimeanza mapema sababu tu mwanamke mwingine tunayefanya kazi naye zake zimeanza,” anaeleza.

Hata hivyo, Bi Bilha anasema kuwa ushirikiano huo humshangaza sana na akaonea fahari mwili wa mwanamke.

“Siku ya kwanza kupata hedhi kwa sababu mwanamke mwingine amepata yake ilikuwa nikiwa shule ya Upili. Niliyekuwa nikiketi naye tulikuwa na siku tofauti za hedhi ambazo zilikuwa zimeachana kwa wiki mbili au tatu. Baada ya muda tukagundua kuwa nimeanza hedhi yangu kwa sababu amepata zake.”

Kwa mshtuko, Bi Bilha aliulizia wanafunzi wenzake na kubaini kuwa ni hulka inayowaathiri wanawake wengi. Hata ingawa hali hii haijabadilika mpaka sasa, Bi Bilha anasema kuwa yeye huhakikisha kuwa kila wakati amebeba sodo kwenye mkoba wake na kufungia pakiti moja dawatini mwake kazini.

“Sasa inanilazimu kujitayarisha kila wakati,” anasema.

Kisa chake si tofauti sana na cha Wambui Nyagai, 27, ambaye anaeleza kuwa ni mamake pekee ambaye huweza kumfanya kuanza kupata hedhi kabla ya siku zake kutimia.

“Kila wakati mamangu anapopata hedhi, mimi pia hupata yangu hata ingawa ilikuwa ije baada ya wiki mbili au zaidi. Huanza siku iyo hiyo au keshoye,” anasema.

Hata hivyo, Bi Nyagai hupokea malalamishi kutoka kwa marafiki wake wa karibu ambao hupata hedhi zao pindi tu wamekuwa kwenye ukaribu naye.

“Sijawahi kosa kuwa na sodo kwenye begi langu kila ninapojua nitamtembelea mamangu,” anasema.

Dkt Moses Kihuga, mtalaamu wa afya ya uzazi katika Kenyatta National Hospital anasema kuwa usawazisho huu wa hedhi ni tukio linalowatokea wanawake ambapo huanza kupata hedhi zao wakati mmoja wanapoanza kuishi pamoja au kuwa kwenye mahusiano ya ukaribu.

“Ingawa hali hii haiwapati wote, wanawake wengi katika umri wa uzazi hushuhudia hali hii. Kwa kawaida, tukio hili huwapata wanawake ambao huishi karibu kwa muda mrefu, ofisini au katika mabweni ya wasichana,” anafafanua.

Japo utafiti kamili haujafanywa kuhusiana na hali hii, Dkt Kihuga anaeleza kuwa homoni ya feromoni huchangia sana hali hii. Homoni hii huonekana hata kwenye wadudu na wanyama kama vile miongoni mwa nyuki, simba na siafu.

“Feromoni ni kemikali zinazotolewa kwenye mazingira na huathiri tabia ya kiumbe mmoja au zaidi katika kundi. Mwanamke “mwenye nguvu zaidi” (dominant female) katika kundi atakuwa na feromoni zenye nguvu zaidi na wanawake wengine wote katika kundi watajaribu kusawazisha mizunguko yao ya hedhi ili kuendana naye,” anaeleza.

Isitoshe, Dkt Kihuga anasisitiza kuwa mwanamke anayeathiriwa na hali hii huwa kwenye hatari kubwa anapokuwa karibu na mwanamke mwingine anayepata maumivu wakati wa hedhi (menstrual cramps).

“Unaweza ukaanza kupata maumivu hayo pia au hata kupata hedhi yako kwa sababu yake.”

Hata hivyo, hakuna madhara ya usawazisho huu wa hedhi kwa afya ya uzazi. Dkt Kihuga anaeleza kuwa hali hii huwa na uhusiano mkubwa na wanawake ambao hupata hedhi zao wakati fulani kila mwezi.

“Wanawake hao huathirika sana ikilinganishwa na wale ambao hedhi zao hazianzi kwa wakati fulani kila mwezi. Hakuna madhara yanayojulikana kwa afya ya uzazi, isipokuwa tu kuvurugika kwa muda ambao mwanamke anapata hedhi zake lakini baadaye hurejea kwenye hali yake ya kawaida au kuwa na mzunguko mpya wa kawaida.”

Pia, Dkt Kihuga anakiri kuwa hakuna data inayoonyesha matukio ambapo mwanamke alipata mimba wakati hedhi zake zilivurugika na kuanza kabla ya wakati wake wa kawaida.

Kutokana mtazamo wa kitabibu, Dkt Kihuga anasema kuwa watu wanapaswa kuelewa kwamba miili ya binadamu imeunganishwa kwa njia isiyoweza kuelezeka kwa urahisi.

“Tumegundua na kujifunza mengi kutokana na miili yetu. Lakini bado kuna michakato ya kifiziolojia ambayo hata wanasayansi hawajaweza kuelewa au kufafanua kikamilifu. Usawazisho wa hedhi ni mmoja wapo.”

  • Tags

You can share this post!

Dereva wa matatu mashakani kwa kuharibu ‘radio call’ ya...

Mudavadi akemea viongozi wa Nyanza kwa ‘kukalia...

T L