• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Munya sasa akujiwa baada ya Oparanya

Munya sasa akujiwa baada ya Oparanya

Na RICHARD MUNGUTI

WANDANI wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga wanaendelea kuandamwa na mkono wa sheria huku kiongozi wa chama cha Party of National Unity (PNU) Peter Munya akiwa wa hivi punde kufikishwa kortini kuhusiana na kesi ya kashfa ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Polisi walifika katika makazi ya Bw Munya na kumfikisha kortini akatoe ushahidi kuhusu kesi hiyo iliyomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na wengine wanane.

Sakata hiyo inahusu ujenzi wa mabwawa ambayo ingegharimu Sh63 bilioni mnamo 2019.
Mahakama ilifahamishwa kuwa Bw Munya ndiye alikuwa “mpuliza kipenga katika sakata hiyo iliyochangia Bw Rotich kukamatwa na kushtakiwa.

Bw Munya hakuwa amefika mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Bi Eunice Nyuttu kesi dhidi ya Bw Rotich ilipotajwa Jumanne wiki jana.

Siku hiyo ndipo Hakimu alimwagiza afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Douglas Chege aeleze alikokuwa Bw Munya.

Bw Chege alisema maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) hawakuwa wamemtia nguvuni Bw Munya kama alivyoagizwa Jumanne wiki hii.
Baada ya simulizi hiyo, Bi Nyuttu aliahirisha kesi hiyo na kumwamuru Bw Munya afike kortini saa tano leo Agosti 31, 2023 ili kesi iendelee.

Saa tano kamili leo asubuhi, Bw Munya alifika kortini na baada ya robo saa hakimu akafika na kuagiza kesi iendelee.

Kabla ya kesi kuanza Bw Munya aliomba msamaha na kufichua “hakuwa amepokea ujumbe kuwa afike kortini Jumanne (Agosti 29 2023).”

Lakini kesi hiyo ilichukua mwelekeo mpya baada ya kiongozi wa mashtaka Oliver Mureithi kuomba iahirishwe akisema,“tunasubiri kiongozi mpya wa mashtaka (DPP) Bw Renson Mulele Igonga apigwe msasa na bunge kisha aapishwe mbele ya Rais William Ruto.”

Pia Bw Mureithi alidokeza kwamba Bw Igonga ataisoma faili hiyo dhidi ya Bw Rotich kisha atoe mwelekeo jinsi kesi itakavyoendelea.

Bw Mureithi aliomba kesi hiyo iahirishwe kusubiri maagizo ya Bw Igonga lakini hakimu akakataa ombi hilo akisema “haki za washtakiwa zinakandamizwa ikitiliwa maanani walifikishwa kortini mara ya kwanza 2019.”

Bi Nyuttu aliamuru Bw Munya aanze kutoa ushahidi lakini Bw Mureithi alisema hana maswali kwa shahidi huyo.

Bw Munya, aliyeharakishwa kufika kortini, alienda nyumbani bila hata ya kusema lolote kuhusu kashfa aliyoifichua.

Baada ya Bw Munya kuondoka kizimbani hakimu alimwamuru Bw Mureithi aite mashahidi wengine lakini “hakuwa nao.”

Mashahidi waliokuwa wameorodheshwa kutoa ushahidi jana ni Bw Munya, aliyekuwa mwanasheria mkuu Profesa Githu Muigai na aliyekuwa mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Bw Edward Ouko.

Mawakili wanaowawakilisha Rotich na wenzake hawakupinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo wakisema “DPP amekumbwa na shida ya kuwafikisha mashahidi kortini huku wengine wakikataa kufika kutoa ushahidi.”

  • Tags

You can share this post!

Mahakama ya Lamu yateketeza dawa za kulevya za Sh2.6 milioni

SHANGAZI AKUJIBU: Mume wangu amefutwa kazi na haniambii,...

T L