• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Mwanafunzi mlemavu afa kwa mkasa wa moto Mukuru-Kayaba

Mwanafunzi mlemavu afa kwa mkasa wa moto Mukuru-Kayaba

NA SAMMY KIMATU

[email protected]

MWANAFUNZI mlemavu wa Darasa la Saba alifariki Jumatatu kwenye mkasa wa moto eneo la Mandazi Road lililo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, South B, kaunti ndogo ya Starehe.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa polisi eneo la Makadara Bi Judith Nyongesa alisema George Muriu aliyekuwa na umri wa miaka 15 alifariki baada ya moto kuteketeza nyumba yao.

Aliongeza kuwa kanisa, stoo ya viatu na makaa na nyumba nne ziliteketea katika kisa hicho cha Jumatatu asubuhi.

Kulingana na babake marehemu, Dominic George Muriu Muga,74, moto huo ulisababishwa na mtu aliyewakisha gurudumu nyuma ya kanisa linalopakana na mto Ngong.

“Nimempoteza mwanangu wa kiume wa pekee. Awali alihusika katika ajali ya barabarani baada ya kugongwa na pikipiki. Ajali hiyo ilimsababishia ulemavu kichwani, mikononi na miguuni. Hata hivyo hilo halikumzuia kuendelea na masomo katika shule ya msingi ya St Catherine iliyoko South B,” Bw Muga alisema.

Aidha, aliambia vyombo vya habari kwamba alifiwa na mkewe miaka miwili iliyopita na ameachwa na watoto watatu wasichana.

Katika eneo la tukio, moshi ulikuwa ukivuka kutoka mvunguni mwa kitanda ambapo marehemu alikutana na kifo chake.

Wakazi wampa pole Mzee Dominic Muga,74, (kati) aliyempoteza mwanawe wa kiume kwenye mkasa wa moto katika eneo la Mandazi Road, Mukuru-Kayaba, South B, kaunti ndogo ya Starehe mnamo Julai, 24, 2023. Kijana George Muriu alikuwa mwanafunzi wa Gredi ya Saba. PICHA | SAMMY KIMATU

Nguo kadhaa zilizoungua za wateja zilidhihirika kwenye kile ambacho zamani ilikuwa sehemu ya kufulia ambapo mzee Muga alijitafutia riziki akifanya kazi ya udobi.

Mtu mmoja aliyeshuhudia mkasa huo ambaye pia ni mwathiriwa, Bw Dominc Muthwii,42, alisema moto huo ulianza dakika chache kuelekea saa kumi na mbili za asubuhi lakini ulikuwa mkubwa na kuchochewa na upepo.

Bw Muthwii alisema ni jambo la kusikitisha kuwa waporaji waliiba mabati yaliyochomeka ambayo yalikuwa yametumika katika ujenzi wa nyumba hizo.

Kutokana na ukosefu wa barabara, hakuna gari la zimamoto ambalo lingeweza kufika katika eneo la mkasa.

Hata hivyo, wenyeji walijizatiti kupambana na moto wakitumia maji kutoka mto Ngong na hatimaye kufanikiwa kuuzima.

Kulingana na mkuu wa tarafa Bw Solomon Muranguri, vijana katika eneo hilo wanastahili pongezi kwa kuwa wepesi na kujituma kuhakikisha moto haukusambaa zaidi kuteketeza nyumba zaidi.

“Nawapongeza vijana wa Kayaba kwa kujitoa na kujituma kuzima moto ndiposa hatukupoteza nyumba nyingi wakati huo. Endeleeni na moyo huo kuokoa maisha yenu na ya wenzenu mtaani. Kaeni na huo undugu,” Bw Muranguri akasema.

Kanisa lililoharibiwa lilitambuliwa kama Kanisa la New Israel.

Bi Nyongesa alisema Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MCA wa Kayafungo awahimiza wakazi kuyahifadhi mazingira

KNCHR yataka maafisa wakandamizaji wa haki wachukuliwe...

T L