• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
MCA wa Kayafungo awahimiza wakazi kuyahifadhi mazingira

MCA wa Kayafungo awahimiza wakazi kuyahifadhi mazingira

NA MAUREEN ONGALA

MWAKILISHI wa Wadi ya Kayafungo katika eneobunge la Kaloleni, Kaunti ya Kilifi, ameitaka serikali ya kaunti na wahisani kusambaza miche mingi ya mitunda kwa manufaa ya mazingira na jamii.

Bi Agnes Sidi alisema kuwa ni muhimu kwa raia kupanda miti ambayo mbali na kulinda mazingira, itawapa wanajamii chakula na pia pesa watakapouza matunda watakayotunda kutoka kwa miti hiyo.

Eneobunge la Kaloleni ni mojawapo ya maeneo nchini yaliyoathirika na tatizo la utapiamlo kwa sababu ya ukosefu wa lishe bora miongoni mwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.

Bi Amina Charo kutoka kijiji cha Kirumbi akipanda mti katika shule ya chekechea ya Kasemeni katika wadi ya Kayafungo. PICHA | MAUREEN ONGALA

Akizungumza katika Shule ya Msingi ya Kasemeni wakati wa kuzindua shughuli muhimu ya kupanda miti milioni moja katika wadi ya Kayafungo, Bi Sidi alisema kuwa eneo hilo limebaki kuonekana kama jangwa baada ya wakazi kukata miti mingi kwa sababu ya kuchoma makaa na kuitumia kama kuni.

“Tunataka kurudisha miti yote iliyokatwa na inayoendelea kukatwa. Eneo hili limebaki jangwa na kila siku bodaboda wanasafirisha maelfu ya magunia ya makaa kuelekea jijini Mombasa, hali ambayo inadhihirisha kiwango kikubwa cha ukataji wa miti. Hatutaki kupanda miche tu ya kawaida, bali miti mingi ya matunda na pia ya kiasilia,” akasema.

Mwakilishi wadi huyo alisema kuwa analenga kuhakikisha ya kuwa Kayafungo itakuwa na miti ya kutosha ndani ya miaka 10 ijayo.

Bi Sidi alisema kuwa analenga kupanda miti mingi katika shule, hospitali, ofisi za serikali na pia kuwapa wazee wa mtaa na Nyumba Kumi miche ili waweze kuitunza miche hiyo hadi kuwa miti mikubwa.

Alisema kuwa analenga kutoa hamasisho kwa wakazi kupenda mazingira na kutunza miti ili hata nao watoto wadogo wazoee kutunza mazingira.

Hii ndiyo maana ameamua kutilia maanani upanzi wa miti katika shule za chekechekea na za msingi.

Kiongozi huyo alisema kuwa licha ya kuwa wakazi hao wameharibu mazingira kwa ajili ya kupata pato la kila siku, hawajanufaika kwa biashara hiyo ya makaa na kuni kwani wanauza kwa bei ya hasara.

“Tunaona bodaboda mmoja anabeba magunia 10 ya makaa lakini bidhaa hiyo haina faida kwani gunia moja ni Sh500 pekee. Kiasi hicho hakiwezi kutimiza mahitaji ya familia kwa wakati huu ambapo gharama ya maisha iko juu,” akasema.

Chifu wa Kinagoni katika eneobunge la Kaloleni Bi Charity Gunga, aliwahimiza wakazi wapande miti katika maboma yao na karibu na vidimbwi vya maji na sio kwa taasisi za serikali peke yake.

Alisema kuwa maeneo ya eneobunge hilo hujulikana kwa kukumbwa na vimbunga ambavyo huharibu nyumba hivyo ni muhimu kupanda miti kuzuia athari za upepo mkali.

Pia mabwawa ya maji katika sehemu hiyo hukauka haraka wakati wa kiangazi kwa sababu hakuna miti ya kulinda maji hayo kutokana na jua na upepo.

Hata hivyo, aliwasihi wakazi wa eneo hilo kutokata miti kwa wingi licha ya kuwa ndio tegemeo.

“Tukiendelea kukata miti kwa wingi ni hatari na itakuwa vigumu kupata tone la mvua siku zijazo,” akasema.

Bw Kuchanja Kaingu alisema kuwa idadi ya miti katika wadi hiyo ilikuwa ndogo na kwa sasa hali imezidi kuwa mbaya kwani wakazi wamekata miti hiyo.

“Sehemu kubwa ya Kayafungo imekuwa kame kwa sababu hatupati mvua kwa zaidi ya miaka minne sasa ndiposa tunachukulia shughuli hii kwa uzito na kutumia mvua kidogo inayonyesha kuanza kulinda mazingira yetu,” akasema.

Alitoa wito kwa wahisani kujitokeza na kusambaza miche kwa wananchi.

Kwa upande wake naibu wa chifu wa Miyami Bi Scholastica Kazungu, alitoa wito kwa wananchi kuunda vijishamba vya miche ili kuwawezesha kustawisha miche mingi.

“Ninawahimiza wananchi wa Kayafungo kuanza kutengeneza mashamba ya miche ili tusiwe watu wa kutegemea kuletewa miche hiyo,” akasema Bi Kazungu.

Alisema kuwa eneo lake limeathirika pakubwa na ukataji miti.

“Tutazunguka kila kijiji katika wadi yetu na kuhimiza kila familia kupanda miti isiyopungua 50,” akasema.

Naye Bw Manyeso Charo ameitaka serikali kuweka sheria ya kutaka kila familia kupanda idadi fulani ya miti ili kurudisha miti iliyoharibiwa na jamii.

“Hali ya mabadiliko ya tabianchi inayozidi kushuhudiwa nchini ina athari kubwa na ni lazima serikali iwe na sheria kali itakayoongeza idadi ya miti kufikia ile asilimia 10,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Tuntigi Gaming wanavyovutia vijana wanaotaka kucheza...

Mwanafunzi mlemavu afa kwa mkasa wa moto Mukuru-Kayaba

T L