• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Mwanamume apatikana amefariki mwili wake ukining’inia chumbani

Mwanamume apatikana amefariki mwili wake ukining’inia chumbani

NA SAMMY KIMATU

POLISI wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamume wa umri wa miaka 30 ulipatikana ukining’inia kutoka paa la nyumba yake huku shingo yake ikiwa imefungwa kwa mshipi.

Akiongea na Taifa Leo mnamo Alhamisi, mkuu wa polisi eneo la Embakasi Bw Wesley Kimeto alisema kisa hicho kilitokea katika eneo la Dakawoo lililoko katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Njenga, kaunti ndogo ya Embakasi Kusini.

Bw Kimeto alisema mwili huo ulitambuliwa kuwa ni wa Bw Wilson Kamande Mwangi.

“Shingo ya marehemu ilikuwa imefungwa kwa mshipi huku vidole vyake vya miguu vikiwa vimegusa sakafu nao mwili ukining’inia kutoka paa la nyumba yake,” Bw Kimeto akasema.

Bw Kimeto aliongeza kwamba mwili huo haukuwa na alama kama ishara ya kushambuliwa kwa kifaa wala hakukuwa na karatasi yenye ujumbe wa kujitoa uhai.

Polisi walichukua mwili na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City huku uchunguzi ukianzishwa na upasuaji ukisubiriwa.

Kulingana na mkewe marehemu, Bi Eunice Njoki, wawili hao walitengana wiki tatu zilizopita kufuatia mzozo wa ndoa.

Baada ya kufarakana, mwanamume huyo aliamua kuondoka katika nyumba yao na kuhamia nyumba nyingine isiyo mbali na kwao.

“Mzee alipata pesa za NHIF Sh20,000 na ndio akashinda akilewa pombe na kuwa mkali,” Bi Njoki alidai huku akilia.

Bi Njeri ameachwa na watoto watatu. Kifungua mimba ana umri wa miaka 19.

Bw Kimeto ameshauri wakazi wa Mukuru-Kwa Njenga na wananchi kwa ujumla kudumisha amani na kutafuta ushauri wa wazee, viongozi wa makanisa na misikiti pamoja na ushauri wa machifu wakati wanatofautiana nyumbani kuliko kujitoa uhai na kuwacha watoto wakiteseka.

“Kuna njia mbadala za kutatua mizozo na kuepuka visa vya watu kujiua, kuna wazee mitaani, Nyumba kumi, machifu na pia viongozi wa kidini ambao ni watu muhimu kutatua tofauti za ndoa ndiposa kuepuka visa vya vifo vya kujitoa uhai,” Bw Kimeto ashauri.

  • Tags

You can share this post!

Mwigizaji Bwire Ndubi aomba msaada wa kifedha kupata...

Jombi alia tangu mke kupandishwa cheo kazini, kabweteka...

T L