• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Omar alitumia ‘juju’ kuzubaisha mpenziwe, korti yaambiwa

Omar alitumia ‘juju’ kuzubaisha mpenziwe, korti yaambiwa

Na RICHARD MUNGUTI

MPENZIWE aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya Keroche Breweries marehemu Tecra Muigai, Omar Lali Omar alitumia juju kumpagawisha kimapenzi.

Bw James Karanja, nduguye Tecra alifichua siri ya mapenzi yasiyo ya kawaida kati ya dadaye na mwendeshaji huyo wa mashua (dau) kisiwani Lamu.

Akitoa ushahidi mbele ya hakimu mwandamizi Bi Zainab Abdul anayechunguza kifo cha kutatanisha cha Tecra kilichotokea Mei 3 2020 , Bw Karanja alisema “dada yangu alinieleza uhusiano wao na Lali ulikuwa sio wa kawaida.”

Bw Karanja alimweleza Bi Abdul kuwa familia imemshikinikiza Tecra auvunje urafiki wake na Lali kwa misingi ya umri.

“Tulimweleza Tecra hawezi kuchumbiwa na Mzee kama Lali ilhali alikuwa na umri mdogo wa miaka 30,” Bw Karanja alisema. Lali alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 50 alipomchumbia Tecra.

Ndugu huyo mkubwa wa Tecra pamoja na rafikiye wa kike Victoria Masela walikuwa wametumwa wasafiri hadi Lamu na mama yao Bi Tabitha Muigai kumshawishi arudi nyumbani na kuachana na Lali.

Mahakama ilielezwa Karanja na Victoria walipatana na Tecra kwenye hoteli moja ya kifahari ijulikanayo Milan kisiwani Lamu.

Tecra alikuwa ameandamana na rafikiye kwa jina Yvonne. Omar alikatazwa kuingia katika hoteli hiyo kwa vile hakuwa amevalia nadhifu.

Ynvone alikuwa anatoka katika familia ya Lali.

Akasema Bw Karanja , “Wakati Tecra alikuwa ametuacha kwa muda kidogo nilimwuliza Yvonne kuhusu maisha ya Lali. Yvonne alifunguka moyo na kunieleza kuwa Lali hakuwa mtu wa maadili mema. Alikuwa anatumia uchawi kuwazubaisha wanawake wampende.”

Yvonne aliendelea kumweleza Bw Karanja kwamba “Lali alikuwa anatumia juju kuwavuta wanawake Wazungu na Waafrika ambao ni matajiri.”

Bw Karanja alisema Tecra alipojiunga nao tena alimshawishi warudi pamoja nyumbani Nairobi. Alikubali lakini baadaye akabadili nia.

Wakati wa mazugumzo yao Tecra alimweleza nduguye, “ kila ninapotaka kumwacha Lali nashindwa kabisa.Sijui huu ni uhusiano wa aina gani. Nikama kuna nguvu za mizimu inayonirudisha kwake.”

Mjakazi wa Tecra , Bi Anne Waithera, akitoa ushahidi alisema wawili hao (tecra na lali) walikuwa wakifarakana kila wakati.

Alidokeza , Tecra alimfukuza Omar Lali mara kadhaa lakini “ akakataa huku akimtisha na kumweleza, siku ile utanifukuza utanijia Lamu aidha ukitembea kwa miguu ama uruke kama ndege.”

“Tecra hakuwa akinificha chochote. Alinieleza mambo yao ya siri na Omar. Alinieleza alikuwa amechoshwa na maisha ya Omar lakini kulikuwa na mvuto usio wa kawaida baina yao. Alikuwa amepagawishwa na Omar kabisa,” Waithera alisema.

Mjakazi huyo alieleza mahakama kuwa, Tecra alimtumia mama yake (Tabitha) picha ya Omar.

“Mama yake alichemka kwa hasira na kumtaka amwache mara moja huyo Mzee (omar). Alikuja hadi kwenye lango la makazi yetu ya kifahari Karagita mjini Naivasha na Tecra akaamuru mabawabu wasimruhusu mama yake kuingia ndani ya nyumba yao,” Waithera alisema.

Mjakazi huyo alisema Omar aliposikia mama ya Tecra alikuwa anakuja kwa makazi yao “alichomoka mbio na kuingia msituni. Alienda kushinda katika ufuo wa Ziwa Naivasha hadi jioni.”

Bi Waithera alisema Tecra alikutana na mama yake katika hoteli moja Naivasha.

“Usiku huo Omar na Tecra walisafiri hadi Lamu na kukaa mle kwa mwezi mmoja,” Bi Waithera alisema.

Bi Abdul alielezwa na mjakazi huyo kwamba Tecra alimweleza asafiri pamoja na mlinzi wake Eric Cheruiyot hadi Lamu.

“Tulipofika Malindi Omar alimpigia Cheruiyot simu na kumwonya atamuua akithubutu kufanya mapenzi nami,” Bi Waithera alisimulia.

Mahakama ilijulishwa, walitoka Malindi wakaenda Lamu kisha wakasafiri kwa mashua hadi visiwa vya Manda ambapo waliishi kwa wiki moja.

Mjakazi huyo aliyekuwa ameajiriwa na Tecra alikuwa anapokea mshahara wa Sh22,000.

Alisema Omar aliwaamuru warudi Naivasha baada ya wiki hiyo moja.

“Tulilala kwa gari Mtito Andei baada ya masaa ya kafyu kutupata hapo tukirudi Naivasha. Tulimpigia simu Tecra hakujibu.Simu zake zote zilikuwa na Omar na ndiye alikuwa anaitikia kama anataka.Tecra alikuwa anaishi kama mfungwa. Hakuwa na uhuru kamwe. Alishinda akilia mchana na usiku kucha.Alinieleza alikuwa anachapwa kama mtoto na Omar,” Waithera.

Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa Omar alikuwa anapokea na kuweka pesa zote ambazo zilikuwa zinatumiwa Tecra kutoka Keroche Breweries.

Bi Waithera alisimulia Omar alikuwa anaalika wanawake Wazungu aliokuwa amezaa nao kumtembelea Naivasha kisha wanalipiwa hoteli walale na Tecra.

“Wazungu wakija na watoto , Omar alikuwa anawafurahisha na kuwaandalia meza kisha Tecra analipa.Jambo hili lilimkera Tecra hata akaapa kumwacha Omar. Alikuwa mpweke kila wakati.Alikuwa anabugia Wine.Usiku walikuwa wanachapana. Kila mmoja alikuwa analala kitanda chake.” Waithera.

Shahidi huyo wa 11 kutoa ushahidi katika uchunguzi huo wa kifo cha Tecra alisema “ Omar alimfukuza kazi na kumwajiri mjakazi mwingine kutoka Lamu.”

Bi Waithera alisema Omar alikataa kumlipa mshahara wake wa Sh44,000 kabla ya kuondoka kazini.

“Alisalia na Sh4,000 hadi wa leo hajanilipa. Alinilipa Sh40,000. Nilianza kazi ya kuuza nguo na pesa hizi,” Waithera.

Mjakazi huyo alisema aliona matangazo kwenye runinga Tecra amekufa.

Mpenziwe Karanja Victoria Masela alieleza alikutana na Omar mara ya kwanza mjini Dar-es-salaam wakati wa sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa ya James.

“Tukiwa Dar Omar alikuwa anakaa peke yake na hakujumuika nasi.Hakuwa anafurahia kutangamana nasi kama familia ya Tecra. Nilimweleza uso kwa uso awachane na Tecra ni msichana mdogo kwa umri naye Omar alikuwa Mzee,” Bi Masela alikumbuka.

Aliendelea kusema alimpokonya mkoba wa Tecra akampa Bw Cheruiyot jambo lililomkasirisha Omar akasema “ wawili hao walikuwa na njama fulani.”

Ni wakati huo Omar alimtishia maisha Cheruiyot kwa kumwambia “nitakufanya utoweke kabisa watoto wako wasikuone tena. Wewe hunifahamu wala hunijui.”

Mahakama imemwamuru Omar afike kortini kujitetea kwa vile yeye ndiye mshukiwa mkuu.

“Kutokana na ushahidi uliotolewa kufikia sasa ni bayana Omar ni mshukiwa mkuu katika kifo cha Tecra. Atahitajika ajitetee na kuwahoji mashahidi waliosalia 33,” aliamuru Bi Zainab.

Mahakama pia imeaamuru mashahidi wengine sita waliompeleka Tecra hospitali kufika kortini Mei 4,2021 uchunguzi utakapoendelea.

Mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai aliamriwa awasake na kuwafikia mashahidi hao sita waliotambuliwa Kasai Lali Omar, Ali Bakari Mohamed, Abdul Akini Lali Omar, Yahya Salim Mohamed, Ahmed Ali Salim na Mohamed Salim Muhanji.

Mahakama ilielezwa sita hao walikataa kufika kortini kutoa ushahidi katika uchunguzi huo wa kubaini kilichomuua Tecra hata baada ya kupelekewa usafiri.

“Walikataa kuabiri gari ya Serikali iliyopelekwa kuwasafirisha hadi Nairobi,” wakili Elisha Ongoya anayewakilisha familia ya Tecra alimweleza hakimu.

  • Tags

You can share this post!

Sonko aondoka hospitalini

MKU kwenye mstari wa mbele katika masuala ya michezo