• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 9:49 AM
Pendekezo mifumo ya kilimo itathminiwe kusaidia kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi

Pendekezo mifumo ya kilimo itathminiwe kusaidia kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi

NA SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Kuangazia, Kutetea Haki na Maslahi ya Mifugo na Wanyamapori Duniani (WAP) limependekeza mifumo ya kilimo na uzalishaji chakula itathminiwe.

Limeonya endapo hatua za dharura hazitachukuliwa, mifumo hatari inayotumika kuendeleza shughuli za kilimo ikalemaza kampeni kukabiliana na athari za tabianchi.

WAP imetaja matumizi ya kemikali za wadudu kwenye mimea na kilimo cha kiwandani, kama mifumo inayohitaji kutathminiwa.

Dkt Victor Yamo, Meneja wa Kampeni Masuala ya Kilimo katika shirika hilo anasema mengi ya maradhi, majanga ibuka yanahusishwa na kutokana na mifumo ya kilimo.

“Kufuatia utafiti, asilimia 26 ya gesi hatari (greenhouse gas) inasababishwa na kilimo. Isitoshe, mifumo tunayotumia kuendeleza ufugaji na kukuza mimea ni kiini kikuu cha maradhi ya afya tunayopambana nayo, asilimia 50 ya majanga ikitokana na mifumo hiyo,” Dkt Yamo afafanua.

Huku mimea ikivuta gesi ya kaboni (Carbon dioxide), mifumo kuendeleza ufugaji inaachilia Methane na Nitrous oxide.

Mwanasayansi huyo vilevile anaonya kuhusu matumizi kiholela ya dawa za antibiotics kwa mifugo, akisema inapunguza kinga ya magonjwa kwa binadamu ikizingatiwa kuwa chembechembe za dawa hizo zinasambazwa kupitia bidhaa kama mayai, nyama, maziwa, na mazao yaliyokuzwa kwa mbolea iliyoathirika.

Huku Kongamano la Umoja wa Mataifa Kuhusu Tabianchi mwaka huu, COP27 likiendelea nchini Misri, ambapo limehudhuriwa na marais na viongozi kutoka dira tofauti za ulimwengu, Dkt Yamo anasisitiza kwamba kampeni kuhamasisha vita dhidi ya athari za tabianchi itafua dafu endapo wakulima watakumbatia mifumo inayodumisha usalama wa mazingira na viumbe.

“Tuanze kwa kupiga jeki wakulima wa mashamba madogo, takwimu zinaonyesha wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula,” aelezea mtaalamu huyo.

Anaoongeza: “Athari za tabianchi ni wazi. Endapo hatutabadili mifumo ya kilimo na ufugaji, Sayansi inasema majanga ya ukame na mafuriko yataendelea kuwa mengi.”

WAP inaendelea kukusanya saini ili kushikiniza serikali za uliwengu kupiga marufuku ya kilimo cha kiwandani, Dkt Yamo akidokeza kwamba watatumia jukwaa la COP28 mwaka ujao kupasha ujumbe.

Barani Afrika, nchi sita zimeonyesha dalili kuunga mkono pendekezo la shirika hilo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mashauriano na maelewano yatamalaki FKF ikianza...

Namwamba ahofia mabadiliko ya tabianchi yatavuruga michezo

T L