• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Mashauriano na maelewano yatamalaki FKF ikianza kunyoosha soka humu nchini

TAHARIRI: Mashauriano na maelewano yatamalaki FKF ikianza kunyoosha soka humu nchini

NA MHARIRI

HAPO jana Ijumaa katibu wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Barry Otieno alitoa ratiba ya msimu mpya wa ligi kuu ya KPL na KWPL, hatua ambayo ilielekea kutoa matumaini ya kukwamuliwa kuimarishwa fani ya soka.

Licha ya dalili hizi za mambo mazuri ambayo yanakuja, kuna tashwishi ambazo zimeibuka baina ya klabu zinazoshiriki kwenye ligi hizo za kitaifa nchini na usimamizi wa FKF.

Mnamo Jumatano, Baraza Kuu ya Shirikisho la Soka Nchini (NEC) ilitangaza kwamba msimu wa ligi uliopita umefutiliwa mbali kwa sababu ulichezwa wakati ambapo Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilikuwa limetoa marufuku kwa kwa Kenya na hivyo, shirika hilo la kimataifa halikuutambua pamoja na matokeo yake.

Kutokana na tangazo hilo, baadhi ya klabu ambazo ziliwekeza katika mechi hizo na kuibuka na matokeo mazuri katika ligi hizo za KPL, KWPL na NSL sasa zinahisi kwamba hazikutendewa haki jasho lao likipuuziliw ambali.

Baadhi ya timu hizo ni kama Tusker FC ambao walitangazwa washindi wa tuzo hilo la ligi kuu msimu uliopita. Timu nyingine ni APS Bomet ambayo iliibuka mshindi katika ligi ndogo ya kitaifa NSL na kuteuliwa kushiriki ligi kuu ya KPL.

Ingawa timu ya Tusker inaonekana kukubali uamuzi wa NEC kufutilia mbali ligi ya msimu uliopita, timu ya APS Bomet imetishia kuelekea mahakamani kusaka haki.

Baadhi ya wadau wa soka nchini walikuwa wamepinga vikali kurejeshwa kwa NEC na waziri wa Michezo Ababu Namwamba kabla ya uamuzi huu kutolewa.

Mfululizo wa vitushi hivi ni ishara kwamba bado kuna msukumano katika usimamizi wa soka nchini na wadai jambo ambalo kwa sasa hivi halifai kupewa nafasi hata kidogo.

Hii ni kwa sababu, Kenya bado inakabiliwa na marufuku ambayo yalitolewa na FIFA, na hivyo basi vita vya aina hii vitaendelea kuchelewesha juhudi za kuondolewa kwa kisiki hiki ili kandanda ya nchi ianze kutamba mara moja.

Ni kwa sababu hii ambapo wasimamizi wa klabu, NEC, FKF na serikali zinafaa kuwa na mashauriano, masikilizano na maelewano haraka iwezekanavyo ili FIFA iondoe marufuku iliyowekea soka ya taifa hili.

Ni lazima wadau wajue kwamba mafanikio yatapatikana ikiwa kila mdau atakuwa tayari kujitolea kupoteza lolote ili kufikia ufanisi huu.

Mfano wa Tusker FC kuwa tayari kushau yaliyopita na kusonga mbele ni wa kuigwa kwa ni ishara ya uzalendo bora.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Aden Duale asije akasahau haki ya...

Pendekezo mifumo ya kilimo itathminiwe kusaidia kuangazia...

T L