• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Polisi Juja wakatazwa kuuza pombe

Polisi Juja wakatazwa kuuza pombe

NA LAWRENCE ONGARO

ILI kudhibiti uuzaji wa pombe za mvinyo, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Juja Bw Charles Mureithi amepiga marufuku maafisa wa polisi kuendesha biashara hiyo.

“Singependa kusikia ya kwamba maafisa wengine wanaendesha biashara ya pombe huku pia wanafanya msako kukamata wafanyibiashara wengine,” alisema Bw Mureithi.

Alisema tayari maafisa wake wameanza kukabiliana na wanaouza pombe katika vituo tofauti hasa katika kijiji cha Witeithie eneo la Juja.

Alisema serikali pia imeanza kusaka matapeli wa ardhi za kuuza ambao wameingilia mali ya umma.

“Tayari nimepokea malalamishi mengi kutoka kwa wananchi kuhusu wizi wa mashamba huku vyeti vya bandia vikitumika. Tayari tunaendelea na msako,” alieleza afisa huyo wa serikali.

Alisema wakazi wa kijiji hicho pia wamelalamikia ukosefu wa umeme kila mara jambo linalokera sana wafanyabiashara.

Wafanyabiashara wengi wanakosa kuhudumia wateja kutokana na ukosefu wa umeme,” alifafanua afisa huyo.

Alitaja maeneo yaliyoathirika sana akisema ni Muthaara, Marava, na Kibute.

Kamanda mkuu wa polisi eneo la Juja Bi Philis Muthoni aliyeandamana na kamishna huyo alisema tayari wanaendelea kumsaka washukiwa wa visa vya ujambazi wanaoua watu kiholela na kutoweka.

“Tumepata malalamiko katika vijiji vya Muthaara na Maraba kuwa watu wengi wanavamiwa usiku na kuuawa kiholela na watu wasiojulikana,” alieleza afisa huyo.

Wakati wa mkutano huo wa baraza mkuu mpya wa polisi Juja Bw John Sankare alijulishwa kwa wakazi hao ili waweze kushirikiana naya kwa maswala ya kudumisha usalama.

“Mimi afisa mpya wa polisi eneo hili niko tayari kufanya kazi nanyi bila mapendeleo,” alijitetea afisa huyo mpya.

Alitoa wito kwa wakazi hao wawe wazi na wajisikie salama huku akiwataka washirikiane naye kwa uwazi.

  • Tags

You can share this post!

Ishara na dalili za upungufu wa vitamini C mwilini

Aliyejifanya askari na kutapeli dereva kizimbani

T L