• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Siasa ndizo mwiba kwa Mumias Sugar

Siasa ndizo mwiba kwa Mumias Sugar

Na MWANDISHI WETU

Hadi miaka ya tisini, Kampuni ya Sukari ya Mumias ilikuwa kampuni tajika yenye tija kuu nchini Kenya.

Ilikuwa kampuni ya sukari iliyosimamiwa vyema zaidi na yenye faida tele kwa wakulima. Mnamo 2003, muda mfupi baada ya ubinafsishaji wake 2001, serikali ilisitisha mkataba wa Booker Tate. Hatua hii ndiyo iliyokuwa kiini cha masaibu ya Mumias Sugar kwa kuwa serikali sasa ilidhibiti usimamizi kamili na kuanza kuteua maafisa wakuu watendaji.

Shida za sasa za Mumias zinatokana na kukosa kulipa mkopo wa Sh540 milioni ambazo inadaiwa na Benki ya KCB. Kampuni hii ya sukari inadaiwa zaidi ya Sh12.5 bilioni na benki.KCB iliweka Mumias Sugar chini ya urasimu mnamo Septemba 2019, jambo lililopelekea wafanyikazi wote kusimamishwa kazi huku ikiunda hasara ya Sh15 bilioni mnamo 2018, kutoka Sh6.7 bilioni 2017.

KCB mwishowe ilichagua kukodisha Mumias kwa wawekezaji kuifufua. Matatizo yalichipuka mara tu habari kuibuka kuwa Devki Steel Mills ndiye mshindi wa zabuni iliyowekwa.Wanasiasa kutoka eneo hilo walianza kuhoji kuhusu mchakato wa ukodishaji.

Hati za mshindi zilitiliwa shaka na siasa hizo zilipelekea kujiondoa kwa mdhamini huyo.Wakati wowote wanasiasa wanapojiingiza katika shughuli ya uwekezaji matokeo yake huwa hasi. Hakujakuwa na natija yoyote baada ya viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali Magharibi mwa Kenya kuingiliwa kisiasa.

Kwa miongo mitatu, wanasiasa kutoka maeneo ya Magharibi na Nyanza wamepambana na majaribio yote ya serikali ya kubinafsisha viwanda vya sukari ili kuvibadilisha na kupata faida.Leo, hakuna hata kiwanda kimoja cha sukari kinachomilikiwa na serikali kinaendeleza shughuli zake ipasavyo.

Kwa nini wadau halisi wa kampuni za sukari wako kimya? Kwa nini wameachia nafasi yao wanasiasa? Kwa nini wasambazaji wa Mumias Sugar, ambao wanadaiwa mabilioni, hawaandai mikutano na kuzungumza kwa sauti moja kupinga dhuluma hii ya kisiasa?Jambo la muhimu sasa ni kujaribu kufufua Mumias Sugar bila ya kuingiliwa kisiasa, kuanza kununua miwa kutoka kwa wakulima, kuuza sukari na mazao yatokanayo na miwa, kuajiri watu, na kuingiza pesa kwenye uchumi wa kieneo na nchi kwa jumla.

  • Tags

You can share this post!

Atokwa jasho jingi viganja vya miguu

Wahamiaji 43 wafariki mashua ikizama