• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Viatu vya Uhuru sasa vyamfinya Rais William Ruto

Viatu vya Uhuru sasa vyamfinya Rais William Ruto

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto amejipata katika hali sawa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta huku akiandamwa au kujipata katika masaibu aliyomlaumu kwa kuyatekeleza au kupuuza.

Kutoka siasa za chama tawala, kukopa madeni, ushuru na miito ya kuwafuta mawaziri na maafisa wa serikali walio washirika wake wa karibu, Dkt Ruto anaonekana kufinywa na viatu alivyovalia Uhuru katika utawala wa Jubilee alipokuwa naibu wake.

Huku chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kikijiandaa kwa uchaguzi wa mashinani mivutano ya ndani kwa ndani sawa na iliyokumba chama cha Jubilee uhuru alipokuwa rais imeanza.

Dkt Ruto anatarajiwa kukutana na maafisa wa chama na viongozi waliochaguliwa kulainisha mambo Ijumaa ijayo.

Mwaka wa 2015 kabla ya Uhuru kuelekea New York kuhudhuria kongamano kuu la Umoja Umoja wa Mataifa, alitofautiana na naibu wake presha zilipozidi awafute kazi mawaziri Felix Koskei( sasa mkuu wa utumishi wa umma) na Davis Chirchir aliyekuwa waziri wa Kawi( ambayo anasimamia katika serikali ya Kenya Kwanza).

Wawili hao walikuwa washirika wa Dkt Ruto na shinikizo hizo zilimfanya atofautiane na mkubwa wake, Rais Kenyatta.
Akiwa rais sasa, Dkt Ruto amejipata katika hali sawa huku naibu wake Rigathi Gachagua akionekana kutofurahishwa na mawaziri na maafisa wakuu wanaotoa kauli zinazofanya serikali kudharauliwa.

Bw Gachagua amekosoa kauli za Bw Kuria na mkuu wa baraza la uchumi la Rais Ruto kuhusu kupanda kwa gharama ya mafuta akisema matamshi yao sio msimamo wa serikali na kuwataka maafisa wa umma kupima maneno yao.

Bw Kuria, ambaye ni waziri wa biashara hakuandamana na ujumbe wa Rais nchini Amerika huku ikisemekana amepigwa marufuku kukanyaga nchi hiyo.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana,Dkt Ruto alikuwa akimkosoa vikali Rais Uhuru kwa kuendelea kukopa kutoka China, kuongeza ushuru na kubebesha Wakenya mzigo wa gharama ya maisha.

Hata hivyo, baada ya kuingia mamlakani, serikali yake imeendelea kukopa kutoka Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kwa masharti makali ambayo yamefanya serikali yake ya Kenya Kwanza kuanzisha ushuru mpya kama wa nyumba, kuongeza ushuru wa ziada wa thamani wa mafuta kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16 hatua ambayo imefanya gharama ya maisha kulemea Wakenya wengi. Ripoti zinasema serikali ya Kenya Kwanza ilikopa zaidi ya Sh1 trilioni katika mwaka mmoja.

Vile vile, serikali ya Rais Ruto imejipata ikilaumiwa na wafanyabiashara kwa sera zinazovuruga mazingira ya biashara Kenya na kutovutia wawekezaji.

Hali hii imekumba sekta nyingi ikiwemo ya kilimo ambapo wakulima wa kahawa na majani chai wanalalamikia sera za serikali walivyofanya chini ya utawala wa Uhuru.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya utawala Solomon Kiore, urais wa Dkt Ruto hauwezi kuwa tofauti na wa Uhuru kwa kuwa waliunda serikali ya Jubilee pamoja. “UDA ni Jubilee B, na inaendeleza sera za Jubilee A. Alichokuwa akifanya Ruto wakati wa kampeni kwa kukosoa Uhuru ni kuongeza nafasi yake ya kushinda urais,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wizi wa mafuta ya transfoma unavyoacha wakazi wa...

Mkenya mashakani Tanzania kwa kuishi nchini humo bila kibali

T L