• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Vijana waliofariki mikononi mwa polisi Embu kuzikwa kwenye kaburi moja

Vijana waliofariki mikononi mwa polisi Embu kuzikwa kwenye kaburi moja

Na SAMMY WAWERU

KAKA wawili wanaodaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi katika hali isiyoeleweka Embu wanazikwa leo, Ijumaa.

Wanazikwa kwenye kaburi moja, nyumbani kwao eneo la Kianjokoma, Kaunti ya Embu.

Vijana Benson Njiru na Emmanuel Mutura, waliaga dunia mapema mwezi huu wa Agosti, baada ya kukamatwa na maafisa wa kituo cha polisi cha Manyatta.

Inasemekana walitiwa nguvuni kwa kukiuka amri ya kafyu.

Miili yao ilipatikana katika hifadhi ya maiti ya Embu Level 5, siku kadha baada ya kukamatwa.

Alhamisi jioni, familia iliandaa maombolezi ambapo mishumaa zaidi ya 500 iliwashwa.

Vijana hao walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu, na maombolezi hayo yalihudhuriwa na wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Huku hafla ya mazishi ya wawili hao ikiendelea katika shule ya Msingi ya Kianjokoma, familia ilitangaza Alhamisi haitaruhusu afisa au maafisa wa polisi kuhudhuria.

Mamlaka ya Kuchunguza Mienendo na Utendakazi wa Maafisa wa Polisi (IPOA) pamoja na kitengo cha masuala ya ndani katika idara ya polisi (IAU), imeanzisha uchunguzi.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i alitembelea familia ya vijana hao Jumatano kuifariji, ambapo aliiahidi kwamba afisi yake itafuatilie kuhakikisha haki imepatikana.

“Nilielezwa kifupi kuhusu kesi na ninasubiri ripoti kamili. Sitaki kusema tutakachofanya, tutafuata sheria.

“Niliahidi baba ya vijana hao tutafanya tuwezalo haki ipatikane na tufuate mapendekezo ya ripoti,” Waziri akaambia vyombo vya habari baada ya kufanya mkutano wa faragha na familia.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki na Inspekta Mkuu wa Polisi, IG Hillary Mutyambai.

Naibu IG, Edward Mbugua wiki iliyopita aliamuru kuhamishwa kwa kwa OCS wa kituo cha Manyatta Adullahi Yaya na OCPD wa Embu Kaskazini Emily Ngaruiya.

You can share this post!

DIMBA PWANI: Ilianza kama Action Boys FC, sasa ni Beach Bay...

KASHESHE: Eti angeishia kuwa dereva wa trela